Friday, December 27, 2013

Viongozi wa ukoo wakerwa Graca kunyanyaswa

Johannesburg, Afrika Kusini. Baada ya mjane wa aliyekuwa Rais wa Kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Graca Machel kutakiwa kuondoka katika familia hiyo na kurudi kwao Msumbiji, viongozi wa ukoo wamewajia juu watoto wa Mandela.

Viongozi hao wa ukoo wa Aba Thembu, wamekasirishwa na kitendo hicho wakisema ni unyama wa kupitiliza wa kumuondoa mjane huyo aliyekuwa akiishi na marehemu Mandela mpaka alipofariki dunia.

Graca alianza kuishi na Mandela baada ya shujaa huyo wa Afrika kuachana mkewe Winnie kutokana na kashfa ya kutokuwa mwaminifu.

Msemaji ukoo huo wa Aba Thembu, Daludumo Mtirara alisema kumwondoa Graca katika ukoo huo ni kosa kubwa kwani bado anastahili heshima kubwa.

“Machel siyo mtu wa kumtukana wala kutumia lugha ambayo si nzuri kwake wala lugha ya vitisho,” alisema kiongozi huyo.

Taarifa za Graca (68), kutakiwa kuondoka nyumbani kwa Mandela zilitolewa na vyombo mbalimbali vya habari vya Afrika Kusini vikiwakariri watoto wa Mandela.

Awali, taarifa zilisema kwamba watoto hao walimtaka mjane huyo aachie mali zote za baba yao na arudi kwao Msumbiji.

“Nkosikazi Nosizwe anatakiwa kuwa ni kiongozi wa familia lakini yeye ndiye anayeongoza kutomheshimu mama yake. Huo ni utovu wa nidhamu,” alisema Mtirara.

Mandela alimuoa Graca ambaye alikuwa mke wa Rais wa Msumbuji marehemu Samora Machel katika sherehe ya kutimiza miaka 80 ya kuzaliwa kwake, Julai 18, 1998.

Rais huyo wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini alifariki dunia Desemba 5 mwaka huu.

-->