Vitambulisho vya wafanyabiashara vyatua Mara

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima leo amegawa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo kwa wakuu wa wilaya za mkoa huo ili nao wawapatie wahusika katika maeneo yao

Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara,  Adam Malima leo Jumatatu Desemba 17, 2018 amegawa vitambulisho vya wafanyabiashara kwa wakuu wa wilaya sita za mkoa huo ili wavigawe kwa wafanyabiashara wadogo.

Amewataka wakurugenzi wa halmashauri na manispaa kuhakikisha walengwa wanapata vitambulisho hivyo ndani ya muda mfupi ili waweze kuendelea na shughuli zao.

“Licha ya kuwa kuna fomu wanazotakiwa kujaza hakikisheni mfanyabiashara hatumii zaidi ya dakika mbili kujaza fomu na kupewa kitambulisho,” amesema Malima na kutaka wenye sifa pekee ndio wapate vitambulisho hivyo.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya za mkoa wa Mara, mkuu wa wilaya ya Tarime,  Glorious Luoga amesema hadi sasa hakuna kikwazo walichokutana nacho katika ugawaji wa vitambulisho hivyo.

Amesema hadi sasa wafanyabiashara 9,000 wameshatambuliwa katika halmashauri tisa za mkoa huo.

“Kwa niaba ya wakuu wenzangu wa wilaya  nawathibitishia kuwa kazi hii itafanyika kwa weledi na ufanisi kwa kuzingatia maagizo na maelekezo yaliyotolewa,” amesema.

Kaimu meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),   Edson Issanya  amesema ofisi yake imeshatoa maelekezo  namna ya kupokea fedha na kuziweka katika akaunti na kutoa risiti kwa wakuu wa wilaya.