Vyama visivyo na wabunge bungeni vyaufagilia muswada wa vyama vya siasa

Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema (kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na muswada wa sheria namba tano wa vyama vya siasa. Anaefatia ni Saum Rashid (Katibu Mkuu UDP) , Abdul Mluya (Naibu Katibu Mkuu DP) na Nancy Mrikaria (Katibu Mkuu TLP). Picha na Muyonga Jumanne

Muktasari:

Vyama vya siasa visivyo na wawakilishi bungeni wawapinga wanasiasa wanaodai marekebisho ya sheria namba tano ya vyama vya siasa utakuwa kandamizi.

Dar es Salaam. Umoja wa vyama vya siasa wasio na wawakilishi bungeni wamewataka wanasiasa, wananchi na wadau mbalimbali kutopotosha juu ya muswada wa marekebisho ya sheria namba tano wa vyama vya siasa uliowasilishwa bungeni.

Muswada huo uliwasilishwa bungeni Novemba 16.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 19, 2018, umoja huo unajumlisha vyama nane, wamesema kitu hicho si kigeni na kilihusisha mawazo ya vyama vyote hivyo ni vyema wasubiri msajili wa vyama ausambaze kwa kuwa ushasomwa bungeni na ni mali ya umma.

Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema amesema wanasiasa wanatumia vibaya muswada huo kwenye mitandao ya kijamii kwa kueleza vipengele vichache ambavyo wanadai vitaathiri vyama.

“Hatutaki kubaki vyama vidogo kila siku, tunataka na sisi tuwe tunashindana kama vyama vingine, basi msajili wa vyama asimamie huu mchakato vizuri ili tupate sheria nzuri na wanasiasa waache kulalamika tusubiri,” amesema Mrema.

Mrema pia amemtaka Rais John Magufuli kuvisaidia vyama vidogo kuwa vikubwa kama ambavyo amekuwa akisaidia katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kwenye zao la korosho.

Naibu Katibu Mkuu wa DP, Abdul Mluya amesema wanaolia kuwa sheria itakandamiza vyama vya siasa wanatakiwa kuwa wavumilivu na wasubiri waupate muswada na kuusoma, kisha walinganishe na maoni waliyotoa.

“Wengi waliotoa maoni hawajapata muswada huu, nashauri wausubiri wausome ndipo wachangie na kulinganisha yale maoni tulitoa kipindi mchakato unaanza mwaka 2013 hadi sasa,” amesema Mluya.

Kadhalika, Katibu Mkuu wa TLP, Nancy Mrikaria amesema sheria hiyo itakuwa na manufaa kwani hapo awali haikutaja mwanamke na ikipita itazingatia usawa wa kijinsia katika siasa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima (AAFP), Rashid Rai amesema wanafurahishwa na uwepo wa sheria kali ambazo zitaongoza vyama hivyo na vitafanya viongozi wa vyama kufanya kazi kwa weledi.

“Nafurahi sana kukiwepo na sheria kali, watu wajue kabla ya kufungia chama kuna onyo ambalo ukikiuka utafungiwa hivyo si kitu cha kulalamika,” amefafanua Rai.

Viongozi mbalimbali wa vyama hivyo wamewatoa hofu wananchi kuwa mchakato huo si mpya na ulisimama kwa sababu mbalimbali ikiwemo Bunge la Katiba mwaka 2014 kisha kurejea tena na wakipata muswada watatoa mapendekezo mengine ili kufanya sheria hiyo kuwa mpya zaidi.