Vyama vya upinzani Tanzania vyatangaza kufanya mikutano ya hadhara

Muktasari:

Vyama sita vya upinzani nchini Tanzania vilivyofanya mkutano wa faragha wa siku mbili visiwani Zanzibar vimetoka maamuzi mawili mazito


Unguja. Vyama sita vya upinzani nchini Tanzania vilivyofanya mkutano wa faragha wa siku mbili visiwani Zanzibar vimetoka maamuzi mawili mazito.

Mkutano huo ulioratibiwa na Chama cha Wananchi CUF chini ya Katibu Mkuu wake,  Maalim Seif Sharif Hamad, vimeazimia kuanza kufanya mikutano ya hadhara kwa kuwa ni haki yao kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.

Pia, wametangaza rasmi kwamba wanasiasa wote waliopo jela kwa tuhuma za kisiasa hao ni ‘Wafungwa wa kisiasa’ na kuanzia sasa wataitangazia dunia hivyo.

Tamko hilo limesainiwa na Maalim Seif, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia; mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi; naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu; mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Vyama hivyo vimetoa uamuzi huo wakati Serikali ya Tanzania ikiwa imepiga marufuku mikutano yote ya kisiasa ya hadhara mpaka mwaka 2020 isipokuwa kwa wabunge walioshinda uchaguzi ambao wameruhusiwa kufanya mikutano kwenye majimbo yao tu.

Miongoni mwa viongozi wa upinzani walio mahabusu ni pamoja na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko ambaye pia ni mbunge wa Tarime Mjini.