Vyama vya upinzani vyatumia siku ya uhuru kudai uhuru

Muktasari:

Vyama hivyo  vilivyoshiriki katika kutoa tamko ni pamoja na ACT Wazalendo, NLD, ADC, Chauma, Chadema, CTK, CUF, UDP, NCCR Mageuzi

Dar es Salaam. Vyama 15 vya siasa vya upinzani vimetoa tamko lao kupinga muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa uliosomwa bungeni Novemba 16 mwaka huu.

Miongoni mwa vyama vilivyoshiriki katika kutoa tamko hilo ni pamoja na ACT Wazalendo, NLD, ADC, Chauma, Chadema, CTK, CUF, UDP, NCCR Mageuzi.

Akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chauma) Hashim Rungwe amesema wameamua kutoa tamko hilo siku ya leo kwa sababu ni siku muhimu ambapo nchi ilizaliwa upya na kuingia katika historia ya kukumbukwa.

“Tumetumia siku hii kwa sababu tunaona dalili za mkoloni mweusi kurejea nchini mwetu na tunampinga ili asiweze kufanikiwa kwa sababu sheria inapendekeza wanasiasa kufanya shughuli zao kwa uhuru lakini hivi sasa jambo hilo linapotea.

“Tumeona nchi nyingi zimeingia katika vurugu kutokana na wao kudai haki zao kwa nguvu ila sisi hatutaki kufanya hivyo ndiyo maana tumeamua kuudai kwa utulivu,” amesema Rungwe.

Amesema sheria hiyo inaweza kuingiza Tifa katika vurugu kubwa siku za baadaye kwa sababu inapinga katiba ya nchi inayotoa uhuru wa kujumuika na kushiriki katika shughuli mbalimbali.