Wachumi watoa angalizo korosho

Muktasari:

Miongoni mwa wachumi hao, DK Haji Semboja amesema Serikali imechukua hatua kwa kuwa wakulima wa korosho  walikuwa wanapata hasara lakini akatahadharisha kuwa suluhisho hilo ni la muda na huenda msimu ujao mambo yakawa kama kawaida kwa kuwa ni soko ndilo litakaloamua bei ya bidhaa hiyo.

Tunduru/Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti kutoka Taasisi ya Repoa, Dk Abel Kinyondo amesema kama mkakati wa kukunua korosho kwa wakulima ulilenga kuwanusuru dhidi ya hasara ambayo wangeipata msimu huu ni jambo nzuri lakini kama ni endelevu linaweza kuleta athari kwa zao hilo na wakulima wa mazao mengine kutaka waiuzie.

“Je, Serikali itanunua bidhaa ngapi, itakuwa na uwezo wa kwenda kote huko. Kichumi bei ya zao lolote inatakiwa iendeshwe kwa mujibu wa soko.”

Alisema korosho inaingiza fedha nyingi za kigeni kuliko zao lingine kutokana na soko lake kuwa la uhakika huku wananchi wa mikoa ya Kusini wakilitegemea kuendesha maisha, “Lakini uuzaji wa zao hilo umegubikwa na siasa jambo ambalo sio zuri. Mwaka jana bei ilifika Sh4,000 kwa sababu Vietnam ambao ni wazalishaji wakubwa walipata hasara baada ya zao hilo kuliwa na wadudu na kusababisha uhitaji kuwa mkubwa sokoni.

“Mwaka huu wamezalisha, ni lazima bei ishuke wale wanasiasa waliojinadi kwa kusema wamedhibiti bei ya korosho inawapa tabu hivi sasa jambo ambalo limelazimisha hatua hizi zichukuliwe,” alisema Dk Kinyondo.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Haji Semboja alisema “Serikali imechukua hatua kwa sababu wananchi walikuwa wanakaribia kupata hasara tofauti na miaka iliyopita. Ila naamini hii ni kwa muda, msimu ujao mambo yatakuwa kama kawaida, soko ndilo litaamua bei ya bidhaa.”

Mwenyekiti wa Jukwaa la Maofisa Watendaji Wakuu (CEOrt), Ali Mufuruki alisema sio mwaka huu pekee ambao Serikali imeweka mkazo katika zao la korosho, bali juhudi hizo zilikuwa zikifanyika tangu zamani japo watu walikuwa hawajui.