Wafanyabiashara waomba kununua korosho

Muktasari:

Wakati serikali ikiendelea na mpango wake wa kununua korosho baadhi ya wafanyabiashara wameomba wanunue korosho hizo ili waendelee na ubanguaji katika viwanda vyao.

Mtwara.  Wakati Serikali ikiendelea na mpango wake wa kununua korosho baadhi ya wafanyabiashara wameomba wanunue korosho hizo ili waendelee na ubanguaji katika viwanda vyao.

Maombi hayo yamekuja baada ya Waziri wa Kilimo na  Umwagiliaji, Japhet Hasunga, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda na mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa kutembelea viwanda hivyo pamoja na kukagua maghala.

Akiwa katika kiwanda cha Micronix mkini Mtwara mmoja wa watumishi wake, Catherine Julius alimwambia waziri ana ombi na kumweleza wanaomba kununua korosho hizo ili wanawake walioajiriwa katika kiwanda hicho waendelee na ajira zao.

“Mheshimiwa waziri tuna ombi, hiki ni kiwanda na zaidi kimeajiri wanawake ambao wana watoto na wengi wao hawana watoto, sasa tuna ombi tunaomba tuuziwe korosho ili tuweze kuendelea na shughuli za ubanguaji na ajira zetu,”amesema Julius.

Hata hivyo, Mkuu wa mkoa huo Gelasius Byakanwa amesema Rais alipoamua kuingilia kati na kununua korosho ilionekana kama ni kuwaonea wafanyabiashara na hawakusikilizwa lakini Serikali ilikuwa makini kuzinunua kwani inajua michezo inayochezwa na wafanyabiashara.

“Waandishi wa habari leo mmekuwa mashuhuda wafanyabiashara wenyewe wakiomba kuzinunua korosho, kwa soko lililopanda lini? Kwa bei ya lini ambayo inaweza kuwalipa? Kwa hiyo ni meseji tosha kulikuwa na mgomo, kwanini leo wanaomba wakanunue korosho kama soko la dunia haliwalipi?”Alihoji Byakanwa.

Aliendelea, “Wale wanaoathirika na ajira kwanza ni masuala ya mkataba na waliowaajiri, lakini Serikali itawahitaji wataalamu wa kubangua korosho ambao ni Watanzania watapata ajira kwenye viwanda vya Serikali ambavyo itavitumia, lakini niwaombe waandishi wa habari mfikishe ukweli walipoomba mlikuwepo na mmeona.”

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Kilimo, Hasunga amesema wakati wanaanza msimu wa ununuzi wafanyabiashara waliweka bei ndogo kwa madai bei katika Soko la Dunia imeshuka jambo ambalo ni kweli lakini si kwa kiwango wanachodai.

 

Amesema baada ya kuapishwa wametumwa Mtwara kuhakiki kwanza kama korosho zipo kwenye maghala na wamehakiki ziko nyingi lakini pia amekutana na wafanyakazi wengi ambao wanafanya shughuli zinazohusiana na korosho.

“Wakati Mheshimiwa Rais alipotangaza bei tulitangaza bei ya kumlipa mkulima, hatukujua kama kuna watu wengine huku ambao wanafanya hiyo kazi na wao wanastahili kulipa, sisi tukajua korosho si zipo.

“Tulipokuja jana nikajifunza kumbe Amcos zinakusanya korosho kwa wakulima na baada ya kukusanya kuna wafanyakazi wengine wanazipokea kutoka kwa wakulima na kuzipakia kwenye magari kuzipeleka kwenye maghala makubwa na wao wanatakiwa kulipwa,” alisema Hasunga.