Wafanyakazi Chuo Kikuu Mount Meru waandamana na mabango hadi kwa Waziri Mhagama

Muktasari:

Wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Mount Meru waandamana na mabango hadi kwa Waziri Jenista Mhagama kudai Serikali kuingilia kati ili  walipwe na chuo hicho malimbikizo ya mishahara yao na stahiki zaidi ya Sh1.1 bilioni.


Arusha. Wafanyakazi 82 wa Chuo Kikuu cha Mount Meru, leo Jumanne Novemba 27, 2018 wameandamana na mabango hadi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakishinikiza uongozi wa chuo hicho, kuwalipa malimbikizo ya mishahara na stahiki zao.

Chuo hicho tayari kimepewa miezi sita ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), kiwe na uwezo wa kifedha kujiendesha na kutimiza matakwa mengine na la sivyo kitafutwa kabisa kudahili wanafunzi.

Wafanyakazi hao wakiwa na mabango ya kudai stahiki zao, walifika kwenye mkutano wa masuala ya maendeleo ya jamii, uliokuwa unafanyika katika hoteli ya Lash Garden jijini Arusha na kutoa malalamiko yao.

Mwenyekiti wa wafanyakazi hao, Emmanuel Sambu amesema licha ya kudai fedha kuna utata juu ya mmiliki halali wa chuo.

Amesema wanadai malimbikizo ya mishahara miezi 10 iliyopita na stahiki zao nyingine Sh1.1 bilioni.

Hata hivyo, amesema wameshangazwa na uongozi wa chuo hicho, kuwataka kuondoka kwa nguvu katika chuo hicho bila ya kuwalipa.

Akizungumza na wafanyakazi hao, Waziri Mhagama ameahidi serikali kuingilia kati suala hilo kuanzia leo Jumanne ambapo kamishna wa kazi na timu yake watafika chuoni hapa kufuatilia madai yao.

Waziri Mhagama amesema Serikali itahakikisha inashughulikia mgogoro huo ili kuhakikisha hakuna haki ambayo inapotea.

Akizungumza na mwananchi, Makamu Mkuu wa chuo kikuu cha Mountmeru, Profesa Johannes Monyo, amekiri wafanyakazi hao kudai malimbikizo ya mishahara na stahiki zao.

Amesema uongozi wa chuo hicho ambacho kinasimamiwa na kanisa la Baptisti Tanzania bado unatafuta fedha za kuwalipa.

Septemba 22, 2018; TCU ilisitisha usaili kwa vyuo vikuu vinne nchini, ikiwapo chuo cha Mount Meru  kutokana na kushindwa kutimiza vigezo ikiwepo kuwa na uwezo wa kifedha  na viliamuliwa kuwaondoa wanafunzi wake wote.