Wahitimu chuo cha TIA wapewa somo

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James

Muktasari:

  • Wahitimu 4,022 wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) wametakiwa kuitumia elimu waliyoipata kujitafutia soko la ajira na kujiajiri

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amewataka wahitimu wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA)  kujiendeleza kielimu ndani ya ajira ili kwenda na kasi ya ukuaji wa teknolojia.

Akizungumza leo Alhamisi Desemba 14, 2018  kwa niaba ya  waziri wa wizara hiyo katika mahafali ya 16 ya chuo hicho amesema  wanafunzi hao hawapaswi kubweteka na elimu aliyoipata, wanatakiwa kutambua kuwa wamevaa kiatu kipya kinachotakiwa kusafishwa kila mara.

Akizungumza mbele ya wahitimu  4,022 amesema, “ninawaasa wanafunzi mnaohitimu ngazi mbalimbali leo  kwamba elimu mnayoipata iwe chachu ya kujiongezea maarifa. Msiwe wataalamu wasio na tija katika kuleta maendeleo.”

Amewataka kutumia elimu waliyoipata kujitafutia soko la ajira na kujiajiri.

“Soko letu la ajira Tanzania ni dogo, ni vyema mkaelekeza mawazo yenu kwenye kujiajiri na si kuajiriwa. Watakaobahatika kuajiriwa jitahidini kufanya kazi kwa bidii na ubunifu na kujiepusha na rushwa,” amesema.

“Mmeanza kuvaa kiatu kipya leo basi msikiache kichakae  endeleeni kujielimisha ili muwe bora zaidi katika soko la ajira.”

Mkuu wa chuo hicho, Joseph Kihanda amesema wkati ya wahitimu 4,022, wanawake ni 2,201 sawa na asilimia 52 na wanaume  ni 1,921 sawa na asilimia 47.8.