Waitara anusa upigaji Dart

Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara akiwa ndani ya gari la mwendo kasi alipotembelea mradi wa mabasi yaendayo haraka (Dart) jana.Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Katika ziara hiyo alitembelea kituo cha mradi huo cha Kivukoni na baadaye kwenda Gerezani ambako alisema yeye binafsi au ofisi yake itafanya tena ziara ndefu ili kubaini changamoto nyingine na ataandaa jukwaa la wadau wote ili kubaini changamoto za pande zote kisha kuzitafutia ufumbuzi.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara ameitaka Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart) kufanya tathmini ya kujua ni hasara kiasi gani Serikali inapata kutokana na mfumo wa utoaji wa tiketi wa sasa katika huduma hiyo.

Waitara alitoa agizo hilo wakati alipotembelea mradi huo jana na kuona tiketi za abiria zikichanwa badala ya kuingizwa (scan) katika mashine kama ilivyokuwa awali jambo ambalo amesema linampa hofu kuwa huenda kuna upigaji unaweza kufanyika.

“Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huu kila mmoja anafahamu, tunataka kila senti hapa ilipiwe kodi na kila kiasi kinachokusanywa kifahamike lakini mashine zikiwa hazifanyi kazi kama hivi napata wasiwasi wa upigaji,” alisema Waitara.

Katika ziara hiyo alitembelea kituo cha mradi huo cha Kivukoni na baadaye kwenda Gerezani ambako alisema yeye binafsi au ofisi yake itafanya tena ziara ndefu ili kubaini changamoto nyingine na ataandaa jukwaa la wadau wote ili kubaini changamoto za pande zote kisha kuzitafutia ufumbuzi.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayotoa huduma katika mradi huo Udart, John Nguya alisema kutokana na mfumo huo kampuni hiyo inapoteza mapato asilimia tatu hadi nne ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Pia alisema kampuni hiyo ina upungufu mkubwa wa mabasi, yaliyopo ni 140 na yanayoingia barabarani ni 127 hadi 130.