Waitara awaweka njia panda Ma-RC, DC, DED

Naibu Waziri wa Tamisem, Mwita Waitara 

Muktasari:

Wanafunzi 133,747 sawa na asilimia 18.24  waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana hawakupata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza  katika shule za sekondari za Serikali mwaka 2019 kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, jambo lililomfanya Waitara kuwatoa hofu wazazi.


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Tamisem, Mwita Waitara amesema kufikia Machi mwaka huu wasimamizi wa elimu wa mikoa ambayo itakuwa imeshindwa kupata madarasa kwa ajili ya wanafunzi wanaotakiwa kuanza darasa la kwanza watakuwa wameshindwa kazi.

Akizungumza leo Alhamisi Januari 10, 2019 jijini Dar es Salaam, Waitara amesema wameshatoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri na wadhibiti ubora wa shule, wakuu wa kanda na wilaya kuhakikisha hadi Machi wanafunzi wote waliochaguliwa wanaendelea na masomo.

“Tumetoa muda hadi Februari na kufikia Machi tutapata taarifa nani ameshindwa na bila kuzunguka nasema atakayeshindwa atakuwa ameshindwa kazi yenyewe na tutawachukulia hatua, hatuna mzaha kwenye elimu, ”amesema Waitara.

Waitara amewataka wazazi kuwa na subira maelekezo ya Serikali ni siku 90 na wameshatoa utaratibu wa kufundishwa wanafunzi watakaochelewa ikiwamo kufundishwa kwa programu maalumu.

“Mzazi ambaye mwanaye hadi kufikia Machi kama kuna mzazi mtoto wake hajaenda shule aje,  halmashauri na ofisi za mkoa  zimejipanga kuhakikisha tunakava hilo,”amesema Waitara.