Wajasiriamali waiangukia TFDA

Baadhi ya wajasiriamali kutoka mikoa ya kusini wakiendelea na mafunzo ya teknolojia mbalimbali ya usindikaji wa bidhaa  yaliyoandaliwa na shirika la viwango nchini (TBS). Picha na Haika Kimaro

Muktasari:

  • Kukosekana kwa nembo ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) katika bidhaa za baadhi ya wajasiriamali kunadaiwa kuwa kikwanzo cha wao kuweza kufikia masoko ya kimataifa

Mtwara. Baadhi ya wajasiriamali wadogo wadogo katika mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara wameiomba Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kuhakikisha wanawawekea nembo katika bidhaa zao ili kuwaondolea hofu walaji.

Wakizungumza katika mafunzo ya teknolojia mbalimbali za usindikaji wa bidhaa yaliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamesema kukosekana kwa nembo ya TFDA katika bidhaa zao kunawasababisha washindwe kufikia masoko ya kimataifa huku kukiwafanya walaji kukosa imani na bidhaa zao.

Wajasiriamali hao wameyasema hayo leo Ijumaa Novemba 16, 2018 wakisema mara nyingi wanapouza bidhaa zao walaji wamekuwa wakihoji nembo ya kutoka TFDA.

“Tunaiomba Serikali katika suala la TFDA wangekuwa wanatuwekea alama kama TBS maana hata mnunuzi anaponunua ukimwambia unayo TFDA anakataa kwa sababu bidhaa haina alama yoyote tunakuwa na cheti chao tu,”amesema Majuma Issa.

Mkuu wA mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amewataka watendaji wa mamlaka kuacha kufanya kazi kwa dhana ya kipolisi polisi na badala yake wawatembelee wajasiriamali kuona mazingira yao ya kazi na kuwashauri ili kuboresha bidhaa zao zifike soko la kimataifa.

“Wewe kama mamlaka ya udhibiti unakaa pembeni kumsubiri aingize bidhaa yake sokoni ndipo umwambie bidhaa zake hazina viwango rudi, tukienda kwa dhana hiyo tunakatisha tamaa, kufifisha jitihada za wajasiriamali, tunafifisha jitihada za wazalishaji,” amesema Byakanwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Athuman Mgenya amesema kwa upande wao wana upungufu wa wafanyakzi lakini bado wanajitahidi kuendelea kutoa elimu kuhakikisha wanawafikia wajasiriamali.

“Tuna taratibu ambazo tumezipanga aende Sido kisha ataelekezwa ni jinsi gani ya kutengeneza bidhaa bora na atapewa barua kuja kwetu basi tunamfanyia shughuli zote kupata nembo bure lakini bado baadhi wamekuwa hawafanyi hivyo,”amesema Dk Mgenya.

Kuhusu gharama za kupata nembo Dk Mgenya amesema: “Kwa wajasiriamali katika miaka mitatu ya kwanza hakuna tozo, gharama tunazikokotoa kulingana na gharama za kufanya uchambuzi na kumfikia lakini gharama zote za Serikali inakuwa imezibeba na hatuangalii tu ubora kwenye bidhaa za kula.”

Mwisho