Wajumbe Bunge la Katiba wafunguka

Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma),Hashimu Rungwe

Muktasari:

  • Mbali na Jaji Warioba na Joseph Butiku, mjumbe wa Bunge la Katiba, Maria Sarungi amesema Katiba mpya ni muhimu ipatikane kwa sababu iliyopo ina viraka vingi na baadhi ya vifungu vinakinzana.


Dar es Salaam. Baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku juzi kusema kuwa mjadala wa kupata Katiba mpya haujafa, baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Bunge la Katiba wameunga mkono kauli hiyo.

Akizungumza juzi wakati wa kumbukizi ya miaka mitano ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC), Dk Sengondo Mvungi, Butiku alisema mjadala wa kupata Katiba hiyo haujafa kwa sababu wenye Katiba ambao ni wananchi bado wanaishi.

Wajumbe hao wamesema suala la Katiba mpya linahitaji kukamilika sasa kwa sababu Watanzania wamesubiri kwa muda mrefu wakisisitiza kuwa itabeba masilahi yao na misingi ya uongozi wa Taifa.

Novemba Mosi, akiwa katika kongamano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais John Magufuli aliweka wazi kuwahakuna fedha kwa ajili ya kuwalipa posho wajumbe ambao watakaa kujadili Katiba mpya na hata fedha zikipatikana zitapelekwa kwenye miradi ya maendeleo.

Siku moja baada ya msimamo huo wa Rais, aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba alisema upo umuhimu wa kuwa na Katiba mpya kwa sababu ni maoni ya wananchi.

Alisema kinachotakiwa ni kukubaliana lini na utaratibu gani utumike kukamilisha mchakato huo.

Akizungumza na Mwananchi jana, mjumbe wa bunge hilo, Maria Sarungi alisema Katiba mpya ni muhimu ipatikane kwa sababu iliyopo ina viraka vingi na baadhi ya vifungu vinakinzana.

Alisema hoja ya maendeleo kwanza kama ilivyobainishwa na Rais Magufuli ina mtazamo wa Mashariki unaoongozwa na China, lakini hilo haliondoi umuhimu wa kuwa na Katiba bora. “Hakuna mtu anayekataa maendeleo, lakini kwanza ni kujenga mfumo na suala hili, haliwezi kufanywa na mtu mmoja. Lazima tuwe na maridhiano kama Taifa, tunataka viongozi wa namna gani, nchi yetu iendeshwe vipi,” alisema.

Akiwa na mtazamo kama huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye alisema Katiba ya sasa ina tofauti kubwa na inayopendekezwa kwenye masuala ya kiuchumi. Alisema masuala muhimu ya kiuchumi yameelezwa vizuri kwenye sura ya pili ya Katiba Inayopendekezwa ikiwamo kumtaka Waziri Mkuu kutoa taarifa bungeni kila mwisho wa mwaka kuhusu hali ya uchumi.

Aliyekuwa mjumbe wa Bunge hilo kutoka Zanzibar, Salma Hamoud Said alisema, “Hili ni suala la wananchi wenyewe, wananchi wanaweza kutafuta fedha kugharamia mchakato wa Katiba yao.”