Wakulima wa korosho 2,168 wajazwa manoti

Waziri wa Kilimo, Japheth Hasunga akizungumza na maofisa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kuhusu mikakati ya ukusanyaji na ununuzi wa Korosho Leo Novemba 17 Mtwara mjini. Kulia kwake ni Mnadhimu wa JWTZ, Luteni Kanali Yacoub Mohammed. Picha na Elias Msuya

Muktasari:

  • Serikali imesema takriban wakulima wa vyama vya msingi 35 vilivyohakikiwa wamepata malipo yao zaidi ya Sh1 bilioni.

Mtwara. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema hadi jana jioni Ijumaa Novemba 16, 2018 wakulima  wa korosho 2,168 kutoka kwenye vyama vya msingi 35 vilivyohakikiwa tayari wamelipwa fedha zao.

Hasunga ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novembea 17, 2018 mjini Mtwara wakati akizungumza na wanahabari kuhusu mwenendo wa malipo hayo na namna korosho hizo zitakavyosafirishwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Katika mkutano huo, Hasunga ameambatana na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Yacoub Mohammed na maofisa wa wengine wa jeshi hilo.

Amesema wakulima hao wameshalipwa zaidi ya Sh1 bilioni na mchakato huo unaendelea katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

"Inawezekana figure (namba) hii ya wakulima waliolipwa ikawa imeongezeka hadi tunavyozungumza sasa (mchana). Bado shughuli inaendelea kuhakikisha wakulima hawa wanapata haki yao," amesema Hasunga.

Katika hatua nyingine, Hasunga amewahakikishia wakazi wa Mtwara waliokuwa wakibeba korosho kuwa ajira zao zipo salama na wasiwe na shaka na ujio wa JWTZ.

"Miongoni mwa kazi zitakazofanywa na jeshi ni kusimamia mchakato wa usafirishaji wa korosho kutoka vyama vya vikuu na kuzipeleka kwenye maghala. Lakini ile ya kubeba na kushusha katika maghala itafanywa na raia wa kawaida," amesema.

Wakati huohuo, Hasunga amesema jana wamefanikiwa kukamata korosho tani 20 zilizokuwa kwenye ghala la Olam zilizokuwa zikipelekwa katika Chama Msingi cha Mnyawi kinyume cha sheria.

Hasunga amesema korosho zinazotoka nje ya nchi hazitapewa nafasi na soko lake halipo, wale watakaobainika kuziingiza kinyume cha sheria watachukuliwa hatua.

Naye Luteni Jenerali Mohammed amesema amepitia Lindi kukagua ghala moja na kiwanda na amefika Mtwara kuangalia namna watakavyofanya katika kutekeleza majukumu yao.