Wakulima wafurahia malipo, vyama vya ushirika taabani

Muktasari:

  • Tayari Serikali imewalipa wakulima 2,168 kutoka vyama vya ushirika 35 huku kukiwa na habari kwamba vyama vya ushirika vitashindwa kujiendesha kwa kukosa mgao vinaostahili kuupata kutokana na malipo ya korosho.

Mtwara. Wakati Serikali ikianza kuwalipa wakulima wa korosho fedha bila makato yoyote, vyama vikubwa vya ushirika mkoani Mtwara vimesema vitashindwa kujiendesha kwa kukosa mgao vinaostahili kutoka katika malipo ya korosho.

Hadi jana mchana, Serikali ilikuwa imeshawalipa wakulima 2,168 kutoka vyama 35 vya ushirika vilivyohakikiwa, huku ikiendelea na uhakiki na kufanya malipo.

Serikali ilifikia uamuzi wa kununua korosho kwa Sh3,300 baada ya wakulima kugomea minada ya awali iliyokuwa na bei chini ya Sh3,000 kwa kilo. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliingilia suala hilo, lakini wafanyabiashara wachache waliojitokeza walinunua korosho kidogo na bei juu kidogo ya Sh3,000.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama vya ushirika vya Tandahimba na Newala (Tanecu) na chama cha Masasi na Nanyumbu (Mamcu), walisema wamekuwa wakijiendesha kupitia makato hayo ya mauzo ya korosho, ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara ya wafanyakazi na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mwenyekiti wa Tanecu, Mohamed Nassoro aliiambia Mwananchi jana kuwa chama hicho kilitarajia kukusanya Sh3 bilioni baada ya kukata Sh30 kwa kila kilo moja katika zaidi ya tani 100,000 walizokusanya.

“Tulipanga kujenga kiwanda kijiji cha Kitangali Tandahimba na ujenzi wa maghala Newala na kulipa mishahara ya wafanyakazi. Haya yote hayatafanyika, tutapata wapi fedha,” alisema Mohamed.

Alisema tayari wameshazungumza na Waziri wa Kilimo, Japheth Hasunga na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, lakini hawajafikia mwafaka.

Maelezo kama hayo yalitolewa pia na mwenyekiti wa Mamcu, Protency Rwiza akisema mpaka sasa hawajui chama hicho kitajiendeshaje.

“Kwa kifupi hatutaweza kujiendesha, ni kama wewe; usipolipwa mshahara utaishije? Huwa tunakata Sh100 kwa kila kilo tunazozitumia kwa mishahara ya wafanyakazi na maendeleo,” alisema Rwiza.

Mbali na vyama hivyo, Shafii Dadi aliyepewa zabuni ya kusafirisha korosho kutoka vyama vya msingi vya ushirika kwenda kwenye maghala wilayani Tandahimba, alisema hajui hatma ya malipo kwa sababu wakulima hawakatwi madeni.

Alisema wameshasafirisha zaidi ya tani 2,000 na bado wanaendelea kwa kuwa wameelekezwa kuendelea wakati suala lao linashughulikiwa.

“Sisi tumepewa tenda na Tanecu, tena kwa mkataba kwa niaba ya vyama vya ushirika vya msingi. Tumekopa fedha benki, tumekodi magari na tunanunua mafuta. Kazi yenyewe ina changamoto nyingi. Kwa mfano leo gari limeharibia, tumekodi jingine ili mzigo wa watu ufike, Lakini mpaka sasa hatujui hatima yetu,” alisema Dadi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana makao makuu ya Bodi ya Korosho mjini Mtwara, Waziri wa Kilimo, Hasunga alisisitiza kauli yake ya kutaka malipo ya wakulima yasiwe na makato yoyote.

“Naomba tuelewane. Tumeichukua hiyo ili mkulima aendelee vizuri. Hii korosho haijauzwa. Tukishauza haya mambo yote kama makato hata ya halmashauri ndiyo tutaangalia. Kwa tafsiri ya sasa, soko limefeli, kwa hiyo sisi tumekuja kurekebisha hali ya soko,” alisema.

“Kwa sasa bei hatujaijua, tukipata bei wote watakuja kulipwa, taasisi zote zilizohusika katika myororo ule wa ujengaji wa bei, tutakaa nao na tutapanga, kila kitu kitaenda vizuri.”

Alisema katika uhakiki wa awali, waliona mkulima anakatwa zaidi ya Sh1,000 jambo alilosema lilikuwa likimuingizia hasara.

“Jana nilikuwa naangalia makato yalikuwa zaidi ya Sh1,000. Kama tungetumia ile bei ya 1,500 mkulima angepata Sh400 tu,” alisema.

Akizungumzia ununuzi wa korosho, waziri huyo alisema hadi jana jioni wakulima 2,168 wa korosho kutoka vyama 35 vya msingi vilivyohakikiwa, walikuwa wameshalipwa fedha zao.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Luteni Jenerali Yacoub Mohammed.