Walalamikia kulipa maradufu Muhimbili

Muktasari:

  • Baadhi ya wagonjwa wamelalamikia malipo maradufu katika Hospitali ya Muhimbili akiwamo mgonjwa mmoja aliyedai kutumia Sh654,220 kwa gharama za vipimo lakini walivyopelekwa Moi ndugu zake walilazimika kulipa upya.

Dar es Salaam. Baadhi ya wagonjwa wanaofika kwa rufaa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamekilalamikia Kitengo cha Dharura (EMD) kuwahodhi kwa muda mrefu kabla ya kuwapeleka sehemu wanakotakiwa, jambo ambalo wanadai huwaongezea gharama za matibabu.

Kwa kawaida wagonjwa wanaopelekwa hospitali hiyo kongwe na kubwa nchini, hufikia kitengo cha dharura ambako shughuli za usajili, upimaji na nyinginezo za awali hufanyika kabla ya mgonjwa kuelekezwa kwenda sehemu inayotoa tiba anayoitaka.

Lakini, ndugu wa wagonjwa wanasema hiyo inasababisha walipie gharama za dharura mara mbili, hasa wale wanaopelekwa Taasisi ya Mifupa (MOI) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

“Tulitoka na mgonjwa wetu Mwananyamala na matatizo ya mgongo, tulipofika Muhimbili tulianzia kitengo cha dharura na hana bima. Hivyo tulikuwa tukilipia cash (taslimu). Ilituchukua siku mbili kupelekwa MOI,” alisema Martin Mongi aliyekuwa amemfikisha mama yake hospitalini hapo kwa matibabu.

Mongi alisema alitumia Sh654, 220 kulipia gharama za vipimo na huduma ya kwanza katika kitengo hicho, lakini walivyopelekwa MOI alilazimika kulipa upya.

“Kitengo cha dharura MOI walituambia lazima wapime upya ndipo wamwanzishie mgonjwa matibabu. Naona utaratibu huu si mzuri, ndugu tunaingia gharama kubwa bila sababu vipimo vilevile mtu anapimwa mara mbili,” alisema.

“Mgonjwa wetu alipata ajali, walimwangalia kama ana majeraha ya ndani eneo la tumbo, kifua na kwingineko waweze kuyatatua kwanza hayo ndipo apelekwe kitengo anachotakiwa,” alisema Victor Manase aliyekuwa anauguza mgonjwa hospitalini hapo.

“Lakini ilichukua siku tatu nasi tulilipia gharama kubwa, alipopelekwa MOI vipimo vilianza upya.”

Wagonjwa wenye matatizo ya moyo ndio wanaolalamika zaidi na wanautaka uongozi wa Muhimbili na taasisi ya JKCI kuangalia namna ya kuwapunguzia gharama.

Wagonjwa ambao wamefikishwa kwa rufaa na ambao wanatakiwa kupelekwa JKCI, hulazimika kupimwa vipimo vya ECHO na ECG.

“Ni bora kama tukaangaliwa hukuhuku JKCI. Sisi tulitoka Mbeya na mgonjwa wetu mwenye tatizo la moyo. Tulianzia pale lakini tulitumia muda mrefu kuja huku. Pale alipimwa kisukari mpaka wakahakikisha imeshuka kwanza ndipo akaanza kupimwa vipimo vya moyo na tulipofika huku alipimwa upya na tukalipia tena,” alisema Adamu Mwamakula, ndugu mwingine wa mgonjwa.

Chanzo cha mapato

Taarifa za ndani zinasema hivi sasa Kitengo cha Dharura hakina chanzo kingine cha mapato isipokuwa kimepewa malengo ya makusanyo kwa kuwa kinajiendesha.

Habari zinasema kuwa wafanyakazi wa kitengo hicho hupata gawio linalowekwa kwenye mshahara wao wa mwezi kulingana na faida waliyozalisha kwa kuwahudumia wagonjwa, hasa wale wa kulipia (IPPM) na wale wa Bima.

Utaratibu huu husababisha wafanyakazi kufanya ‘kila liwezekanalo’ kuhakikisha wanatunisha mfuko wao.

Hata hivyo, mkuu wa Kitengo cha Dharura, Dk Juma Mfinanga amekanusha taarifa kuwa kitengo hicho kinajitegemea kifedha na kuwalipisha wagonjwa ili kipate fedha za kujiendesha.

“Si kweli, hatufanyi biashara yoyote hapa. Zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa hapa hawalipi na hatuna sababu yoyote ya kuweka gharama, hospitali yetu inatoa huduma na haifanyi biashara,” alisema Dk Mfinanga.

“Sehemu ya dharura wataalamu wanahitaji muda kukaa na mgonjwa na kuna siri ndiyo maana tunaomba ndugu wasubiri nje ili mgonjwa aseme tatizo lake kwa daktari ili atibiwe kile anachoumwa.”

Naye Dk Mfinanga anasema zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa wanaofika Kitengo cha Dharura hawalazwi na hurudi nyumbani lakini hakuna muda maalumu wa kitengo kukaa na mgonjwa isipokuwa hali yake ndiyo huamua.

“Daktari atasema mgonjwa huyu anahitaji uchunguzi wa daktari tofauti wa kitengo fulani na kitengo hicho ama kiwe hapa hapa Muhimbili au taasisi nyingine zilizopo ndani ya Muhimbili.

Anasema kazi ya EMD ni kuhakikisha inaokoa maisha ya mgonjwa na kuhakikisha amekaa sawa kabla ya kumpeleka katika kitengo husika.

Rufaa hutolewa kimakosa

Lakini mkurugenzi wa MOI, Dk Respicious Boniface alisema si kila mgonjwa anatakiwa apitilize kitengo cha mifupa.

“Wapo ambao hupewa rufaa kimakosa. Unakuta ameandikiwa MOI kumbe alitakiwa kwenda JKCI au eneo jingine, hivyo akipita pale atapatiwa vipimo upya kubaini anafaa kupelekwa wapi,” anasema.

Hata hivyo, Dk Boniface anakubali kuwa utaratibu wa wangonjwa kupelekwa moja kwa moja vitengo husika utasaidia kupunguza gharama.

“Wagonjwa wakifika Kitengo cha Dharura watapimwa vipimo vyote, na iwapo ataletwa huku, sisi pia lazima tupime vipimo vyote kujiridhisha ili tumwanzishie matibabu. Hapo wagonjwa wanalipa gharama mara mbili,” alisema.