VIDEO: Waliofukuzwa uanachama CCM wasamehewa, Mtolea apitishwa kuwania ubunge Temeke

Stephen Wasira akipigwa picha ya pamoja na wafuasi wa Chama hicho wakati akiwa katika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Leo Jumanne Desemba 18, 2018 Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kimewasamehe na kuwarejeshea uanachama  waliokuwa wenyeviti wa mikoa wa chama hicho huku kikimpitisha Abdallah Mtolea kuwania ubunge wa Temeke. Awali Mtolea alikuwa mbunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF


Dar es Salaam. Halmashauri Kuu ya CCM imewasamehe na kuwarejeshea uanachama  waliokuwa wenyeviti wa mikoa wa chama hicho tawala nchini Tanzania.

Waliosamehewa na mikoa waliyokuwa wakiiongoza katika mabano ni Ramadhani Madabida (Dar es Salaam), Erasto Kwirasa (Shinyanga), Christopher Sanya (Mara) na Salum Madenge ambaye alikuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni.

Kikao hicho cha Halmashauri Kuu kilichoongozwa na mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli pia kilipokea taarifa kuhusu masuala ya maadili, utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 18, 2018 katika kikao na waandishi wa habari Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema msamaha huo ni sehemu ya maazimio ya kikao hicho kilichofanyika Ikulu, Dar es salaam.

Kikao hicho pia kimepitisha jina la Abdallah Mtolea kuwania ubunge wa Temeke. Awali Mtolea alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF.

“NEC imepitisha majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM. Ni katika ngazi za wilaya, mkoa na Taifa zilizoachwa wazi baada ya waliokuwa katika nafasi hizo kupangiwa majukumu mengine ya serikalini au kufariki dunia,” amesema.

Hata hivyo,  kikao hicho kimemuweka chini ya uangalizi usiokuwa na kikomo aliyekuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu ambaye ameomba kurejeshewa uanachama.