Waliojiuzulu Ubunge Chadema, waapishwa kuwa wabunge wa CCM

Muktasari:

  • Wabunge  waliohamia  CCM kisha kushinda nafasi hizo bila kupingwa, wameapishwa leo Alhamisi na Spika Job Ndugai

Dodoma. Spika Job Ndugai leo Alhamisi Novemba 15, 2018 amewaapisha wabunge wa nne wa Chama cha Mapinduzi.

Wabunge hao ni James Millya (Simanjiro), Joseph Michael Mkundi (Ukerewe), Pauline Gekul (Babati Mjini) na Ryoba Marwa (Serengeti) ambao walipita katika majimbo yao bila kupingwa.

Kabla ya hapo uchaguzi wa majimbo hayo ungepaswa kufanyika Desemba 2,2018 na Spika wa Bunge akizungumza na waandishi wa habari Novemba 5, 2018 alisema wabunge hao wanne licha ya kupita bila kupingwa wangeapishwa mkutano wa 14 mwakani.

Wabunge wa upinzani hawakuwepo wakati wanaapishwa wabunge hao ambao wote walikuwa Chadema kabla ya kuhamia CCM ambako walipitishwa kugombea nafasi hizo.

Mara baada ya kumaliza kuwaapisha, Spika Ndugai amesema, ‘Nne bila’ huku shangwe kutoka kwa wabunge wa CCM zikiibuka wakati.

Wabunge hao kila mmoja, alipokuwa akiingia kuapishwa, walisindikizwa na wabunge wa CCM ambao walikuwa wakishangilia.

Baada ya kumaliza kuapishwa, wabunge wa upinzani wamerejea bungeni.