Waliouza korosho bila mashamba kuambulia patupu

Mkuu wa Wilaya Nachingwea, Rukia Muwango

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya Nachingwea, Rukia Muwango  amesema waliouza korosho bila kuwa na shamba la zao hilo wajiandae kisaikolojia kwani hawatalipwa.

Nachingwea. Mkuu wa wilaya Nachingwea Rukia Muwango amesema wafanyabiashara  walionunua korosho nje ya mfumo rasmi humo hawatalipwa kwakuwa hawana mashamba.

Muwango alibainisha hayo jana Jumamosi Desemba 8, 2018 jioni  akihutubia mkutano wa hadhara kijiji cha Farm 17.

Alisema Serikali haikusudii kumdhulumu mtu lakini haipo tayari kuwalipa watu walionunua zao hilo nje ya  mfumo rasmi maarufu Kangomba.

Alisema zoezi la uhakiki linaloendelea linafanywa kwa umakini na uhakika bila kumuonea mtu.

“Lengo la zoezi hili ni kuwatambua wakulima halali wanaostahili kulipwa na wale walionunua kwa kangomba na kuwadhulumu wakulima hawatalipwa. Wajiandae kisaikolojia kupata hasara, fedha za Serikali haziliwi hovyo,” amesema.

Alisema badala yake, fedha ambazo wangelipwa zitapelekwa kwenye miradi ya maendeleo.

Alisema watu waliokodi mashamba wasiwe na hofu ya kupoteza haki yao.