Walipa mamilioni kukwepa kifungo cha miaka miwili jela

Muktasari:

  • Mfanyabiashara Kamaljit Hanspaul (58) na raia watatu wa kigeni wamehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kulipa faini ya Sh60 milioni  au kwenda jela miaka miwili kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kuajiri na kufanya kazi nchini bila vibali

Arusha. Mfanyabiashara Kamaljit Hanspaul (58) na raia watatu wa kigeni wamehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kulipa faini ya Sh60 milioni  au kwenda jela miaka miwili kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kuajiri na kufanya kazi nchini bila vibali.

Wengine waliohukumiwa ni Kumar Vemula (27) raia wa India, Vinoth Krishanth (29) raia wa  Sri Lanka na Raiph Leopold Hruscka (54) raia wa Ujerumani.

Hata hivyo, washtakiwa wote walilipa faini hiyo na kukwepa kifungo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Niku Mwakatobe akisoma hukumu hiyo alisema Novemba 12 washtakiwa hao walikutwa kwenye kampuni ya Hanspaul Automech wakifanya kazi bila kuwa na vibali.

Alisema Mahakama hiyo imetoa adhabu kwa Hanspaul kulipa faini ya Sh30 milioni kwa makosa matatu ya kuajiri wafanyakazi watatu wa kigeni bila kuwa na vibali vya kazi au kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani .

Washitakiwa wengine watatu wamepewa adhabu ya kulipa faini ya Sh10 milioni  kila mmoja kwa kosa la kufanya kazi nchini bila kuwa na vibali vya kazi au kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani.

Kabla ya hukumu hiyo, wakili wa Serikali, Khalili Nuda aliwasomea mashtaka yao washtakiwa hao na walikiri kufanya makosa hayo.

Wakili wa utetezi,  Salimu Mushi aliiomba Mahakama kuwapunguza adhabu wateja wake kwa sababu ni mara ya kwanza kukutwa na hatia, akidai raia hao wa kigeni walikuwa wakifuatilia vibali vyao.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 4 mwaka huu na kusomewa mashitaka huku Vemula

na Hruscka wakielezwa kuwa walikuwa wanafanya kazi kwenye kampuni  ya Hans Paul Automech  kama wahandisi washauri wa kiwanda hicho na Krishanth  alikuwa akifanya kazi ya uhandisi wa magari.