Wamachinga wafurahia vitambulisho

Muktasari:

  • Utaratibu wa usajili wa wafanyabiashara ndogo unafanyika katika nchi nyingi duniani, mathalani Ubelgiji imewasajili wafanyabiashara wote wadogo katika miji ya Brussels, Antwerp, Anderlecht na Ghent.

Dar es Salaam. Baada ya Rais John Magufuli jana kutangaza kutoa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo na kuagiza wasibughudhiwe, wajasiriamali hao wamepongeza hatua hiyo na kuahidi kumuunga mkono.

Aliyekuwa katibu wa umoja wa wamachinga katika Soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya, Ipyana Kipyo alisema endapo kero zao zitasikilizwa na kutatuliwa vitambulisho 25,000 vitakwisha haraka.

Vitambulisho hivyo vinatolewa kwa malipo ya Sh20,000 kila kimoja lengo likiwa ni kuwatambua wafanyabiashara hao

Kipyo alisema, “Machinga wa Mbeya biashara zao hazijatulia hivi sasa, hatuna sehemu maalumu ya kufanyia biashara zetu na kila siku tunakimbizana na vijana wa JKT, jambo hilo huenda likakwamisha uuzaji wa vitambulisho hivyo, vinginevyo hatuna tatizo.”

Alisema wamachinga wa jiji hilo waliwahi kuiomba Serikali wawe wanalipa kodi na ushuru kwa masharti ya kutobughudhiwa, lakini viongozi walikataa na kwamba wakipewa eneo ambalo hawabughudhiwi itabidi vitambulisho zaidi viongezwe siku inayofuata.

Fred Paul, mfanyabiashara ndogo wa nguo za kike Tabata jijini hapa, alisema anasubiri kwa hamu kitambulisho na akapongeza hatua hiyo kuwa ni nzuri.

“Tumekuwa tukisumbuliwa utadhani tunauza dawa za kulevya wakati tunatafuta riziki. Binafsi nasubiri vifike na nitanunua kitambulisho changu siku hiyohiyo ili nifanye biashara zangu kwa uhuru,” alisema Paul.

Kutoka jijini Dodoma, Emmanuel Nzoya anayeuza urembo mchanganyiko alisema anaunga mkono utaratibu alioutaka Rais ili kufanya biashara zake kwa uhuru.

“Kama biashara inafanyika bila bughudha Sh20,000 ni kiwango kidogo kuchangia kwa mwaka. Wamachinga wengi hapa Dodoma hilo lipo ndani ya uwezo wao,” alisema Nzoya.

Jana, Rais Magufuli aligawa vitambulisho 670,000 kwa wakuu wa mikoa nchini kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ambavyo aliagiza vitolewe kwa malipo ya Sh20,000 kila kimoja na kila atakayekuwa nacho asisumbuliwe. Kila mkoa umepewa vitambulisho 25,000.

Kwa kipindi kirefu, Rais alisema amekuwa akiiagiza TRA na halmashauri kutowatoza kodi wajasiriamali wadogo ambao mitaji yao haizidi Sh4 milioni, lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua. Utambuzi wa wamachinga ulianza mwanzoni mwa mwaka huu ukisimamiwa na TRA, lakini kutokana na vitambulisho hivyo kuunganishwa na vile vya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Rais alisema vinawakimbiza baadhi ya wafanyabiashara wadogo.

“Hakuna ulazima wa kuviunganisha vitambulisho vya wamachinga na Nida, kwani siyo lazima kila anayefanya biashara awe Mtanzania. Mkigundua kuwa si raia, tafuteni muda mkamkamate,” alisema Rais Magufuli.

Alizitaka halmashauri na mamlaka za usimamizi kutomgusa mjasiriamali atakayekuwa amevaa kitambulisho alichotoa ambacho kinamruhusu mfanyabiashara kuendelea na shughuli zake mahali popote nchini.

Utaratibu wa kuwatambua wafanyabiashara wadogo ulipitishwa na Bunge kwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 ambayo licha ya kuwatambua kulingana na sehemu wanazofanyia biashara, inawapa fursa ya kulipa kodi kuchangia uchumi wa Taifa.