Wamiliki viwanda vya korosho waiangukia Serikali, JWTZ watua kuzisomba

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa akisalimiana na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kabla ya kukabidhiwa magari matano kati ya 75 yatakayotumika kusafirisha korosho. Picha na Haika Kimaro

Muktasari:

  • Wamiliki hao akiwamo wa Kiwanda cha Hawte Investment Ltd chenye wafanyakazi zaidi ya 600, wameiomba Serikali kuwauzia korosho ili kuendeleza uzalishaji pamoja na kulinda ajira za watumishi wao.


Mtwara/Newala. Wakati Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa akipokea magari matano kati ya 75 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa ajili ya kusomba korosho, baadhi ya wamiliki wa viwanda wameiangukia Serikali wakitaka iwauzie korosho.

Wamiliki hao wameiomba Serikali kuwauzia korosho hizo ili kuendeleza uzalishaji pamoja na kulinda ajira za watumishi wao.

Meneja wa kiwanda cha Hawte investment Ltd kilichopo Mtwara mjini, Sadat Abdul alisema wameajiri zaidi ya wafanyakazi 600 na muda si mrefu watakifunga kwa kuwa korosho zimekwisha.

“Siyo kwamba tuligoma kununua korosho, ila bado tulikuwa tunajipanga ikiwa ni pamoja na kushughulikia mikopo ya benki,” alisema.

“Hata hizi korosho tunazomalizia tulizinunua Desemba mwaka jana wakati msimu unaanza Oktoba. Tunaiomba (Serikali) ituuzie tu kwa sababu hata leseni tulishakata.” Juzi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Byakanwa alihoji ni kwa nini wafanyabiashara hao wanaomba wauziwe hivi sasa, ilhali awali walisuasua.

Jeshi latua kusomba

Jana, mkuu huyo wa mkoa alipokea magari matano ya JWTZ ili yatumike kusomba korosho kutoka katika maghala ya vyama vikuu vya ushirika kwenda katika maghala yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuhifadhia.

Wiki iliyopita, Rais John Magufuli alikagua magari hayo na kumwagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo kuyapeleka Mtwara kwa ajili ya kazi hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhiwa magari hayo, Byakanwa alisema magari zaidi yatapokewa na kuwataka makuli wanaopakia na kupakua magunia yenye korosho kuondoa wasiwasi wa kupoteza ajira zao.

Juzi, wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya makuli walionyesha hofu ya kupoteza vibarua vyao baada ya Serikali kutangaza kununua korosho zote. Baadhi ya makuli waliokutwa katika ghala la Olam mjini Mtwara, walisema msimu huu umewaendea vibaya tofauti na miaka iliyopita korosho zilipokuwa zikinunuliwa na Wahindi.

Hata hivyo, Byakanwa alisema, “Wale wote ambao kwa msimu huu kazi yao kubwa ni kubeba magunia na kupakia kwenye malori tumesema hatutawafukuza, tutakubaliana nao kuweka utaratibu kuhakikisha na wao wanaweza kushiriki ili kupata kipato.”

Akizungumzia kuanza kazi ya kuwalipa wakulima, mkuu huyo wa mkoa alisema uhakiki wa majina yao umemalizika na sasa wanahakiki akaunti zao za benki. “Baada ya malipo kufanyika hatua inayofuata ni magari ya jeshi tuliyoyapokea kuanza kusafirisha korosho toka kwenye maghala makuu kwenda kwenye maghala ya kuhifadhia.”

Tayari kikosi cha wanajeshi 20 kimewasili wilayani Newala na kupokewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Aziza Mangosongo aliyewatembeza katika maghala matatu makubwa ya kuhifadhi korosho.