Wanafunzi 5,000 Manyara uhakika kuendelea kidato cha kwanza

Muktasari:

Wakurugenzi Manyara watakiwa kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu kwenda sekondari wanajiunga na kidato cha kwanza mwakani.

Babati. Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Missaile Mussa amewaagiza wakurugenzi  na watendaji wa Halmashauri za mkoa huo kuhakikisha wanafunzi 5,000 waliokosa nafasi baada ya kuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza,  wanaanza masomo mwaka 2019.

Mussa ameyasema hayo mjini Babati jana Jumamosi Desemba 15, 2018 katika kikao cha kamati ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mwakani.

Amesema ni haki ya wanafunzi hao kuendelea na masomo kwa kuwa wamechaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.

"Hakikisheni wanafunzi wote waliochaguliwa wanaendelea na sekondari kwa sababu hata muda umebaki mfupi,” amesema.

Ofisa elimu wa Mkoa wa Manyara, Anorld Msuya amesema wanafunzi 21,453 sawa na asilimia 70.79 ya waliofanya mtihani wa darasa la saba wamefaulu.

Amesema  16,061 sawa na asilimia 74.87 ya waliofaulu watapata nafasi ya kuanza  kidato cha kwanza mkoani humo.

Amesema kuna shule za sekondari za kutwa 137 zinazochukua wanafunzi 19,950, wavulana 9,475 na wasichana 10,475.

Amesema shule za bweni zipo 105 na wanafunzi wengine watakwenda kwenye sekondari za Pugu, Malangali, Balangdalalu na Ifunda.