Wananchi watakiwa kuwekeza katika mapori

Muktasari:

Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi watakiwa kutumia fursa za kupandishwa hadhi kwa mapori ya akiba ya Buligi, Biharamulo, Kimisi, Ibanda na Rumanyika kwa kuwekeza kwa kujenga hoteli za kitalii na vivutio cha asili.

Chato. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amesema kupandishwa hadhi kwa mapori ya Buligi, Biiharamulo, Kimisi, Ibanda na Rumanyika ni fursa  za kiuchumi kwa wakazi wa kanda ya ziwa,  hivyo ni vyema wakaitumia fursa hiyo kwa kujenga hoteli za kitalii na kuwa na vivutio vya asili.

Akizungumza wakati wa mashindano ya Rubondo Marathon yaliyofanyika Disemba 9,2018 wilayani Chato mkoani Geita yenye lengo la kutangaza vivutio vilivyopo katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo, Naibu waziri alisema kupandishwa hadhi kwa hifadhi hizo ni fursa kiuwekezaji.

Amesema  wafanyabiashara wanaweza kujenga hoteli za kitalii, kuwa na magari ya kubeba watalii pamoja na kuwa na vivutio vya asili ambavyo vitawawezesha kujipatia kipato cha kaya na Taifa kwa ujumla.

Kanyasu amesema sekta ya utalii nchini imekuwa ikitoa ajira mbalimbali ambapo kwa mwaka 2017 sekta hiyo imeajiri watu zaidi ya 500,000 ambao ni sawa na asilimia tatu ya ajira zilizopo nchini huku ajira zisizo za moja kwa moja zikiwa zaidi ya 1,500,000.

Amesema hadi kufikia mwaka 2028 sekta ya utalii itakuwa imeajiri watu zaidi ya 1.9 milion na kusema uwekezaji kwenye uhifadhi ili kuhamasisha utalii ni jambo la kipaumbele katika uchumi wa nchi.

Mhifadhi mkuu wa Rubondo Ignas Galla amesema utalii wa ukanda wa kaskazini magharibi utaleta wageni wengi kutoka nchi za Uganda ,Rwanda na Burundi.