Wanasheria wajadili suala la kumshtaki Rais

Muktasari:

Wakili aliyekabidhiwa jukumu hilo asema tayari amelifikisha mahamani anasubiri taratibu

Siku moja baada ya katibu wa itikadi, uenezi na mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu kueleza dhamira yake ya kufungua kesi dhidi ya Rais John Magufuli, wanasheria wametoa maoni yao kuhusu suala hilo.

Uamuzi wa kumshtaki Rais umefikiwa kwa kile kilichodaiwa kuwa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi ulikiuka sheria.

Shaibu aliwaambia wanahabari juzi kuwa Dk Kilangi hana sifa na Rais Magufuli alikiuka matakwa ya Katiba kwa kumteua kushika nafasi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume alisema sheria inasema Rais anaweza kushtakiwa iwapo atakiuka Katiba au atafanya kosa la madai.

Hata hivyo, mhadhiri wa Chuo wa Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Onesmo Kyauke alisema Rais anaweza kushtakiwa lakini kwa kupitia kwa AG.

“Hawa viongozi wa juu, Rais, makamu wake, waziri mkuu nk. wanapofanya makosa wanashtakiwa lakini kupitia kwa AG kwa kuwa yeye ndiye anayehusika na kesi zote za Serikali,” alisema.

Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju alisema hawezi kulizungumzia kwa kuwa halijafikishwa rasmi serikalini.

Karume alisema hatua ya kumshtaki Rais Magufuli imefikiwa baada ya kuonekana hashauriki.

“Mwanasiasa anatakiwa kusikiliza ushauri na matakwa ya wananchi. Hakuna namna ya kulitatua zaidi ya kwenda mahakamani,” alisema Karume.

Karume, ambaye ndiye wakili wa Shaibu katika kesi hiyo, alisema tayari amewasilisha hati ya mashtaka na Mahakama imeipokea wanasubiri taratibu nyingine za kimahakama.