Wapinzani nchini wataja sababu mpinzani DRC kushinda urais

Muktasari:

Wakati macho na masikio yakiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 30, 2018, tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imemtangaza mgombea wa upinzani kuwa mshindi

Dar es Salaam. Wakati wimbi la upinzani likizidi kushika madaraka barani Afrika baada ya Felix Tshisekedi kushinda uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia na Congo (DRC), viongozi wa vyama vya siasa nchini wamesema matokeo hayo yanatokana na tume ya uchaguzi kuwa huru pamoja na mshikamano wa wananchi.

Tume ya Uchaguzi ya DRC (Ceni) ilitangaza ushindi wa Tshisekedi jana alfajiri baada ya uchaguzi uliofanyika Desemba 30 mwaka jana.

Hata hivyo, mgombea mwingine wa upinzani aliyeshika nafasi ya pili, Martin Fayulu amepinga matokeo hayo, akiyaita kuwa ni “mapinduzi ya kura” na kuungwa mkono na Ufaransa, ambayo inasema mshindi halali ni mgombea huyo wa muungano wa vyama vya upinzani, UNC.

Ceni ilitangaza kuwa Tshisekedi wa chama cha UDPS amepata kura milioni 7 ambazo ni sawa na asilimia 38 ya kura zote, akifuatiwa na Fayulu wa UNC (milioni 6.3) huku Emmanuel Ramazani Shadary wa chama cha rais Joseph Kabila akipata kura milioni 4.3.

Ceni ilichelewa kutangaza matokeo hayo ya awali, jambo lililosababisha kuzuka kwa vurugu mitaani.

Hata hivyo, viongozi wa upinzani nchini wamepokea matokeo hayo kwa kuisifu Ceni.

“Licha ya uchaguzi kugubikwa na sintofahamu siku chache kabla ya kupiga kura hadi taasisi hizi kupaza sauti, imeonekana jinsi mshikamano ulivyo na nguvu katika maaamuzi ya mambo ya haki na kudai demokrasia,” alisema John Mrema, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema.

Mrema pia alisema mshikamano ulioonyeshwa na taasisi mbalimbali za serikali na kidini nchini humo, umechangia kwa kiasi kikubwa katika ushindi huo.

Alisema jambo hilo linapaswa kuigwa na nchi nyingine za Afrika kwa sababu licha ya tume hiyo kuwa chini ya uongozi wa chama tawala, ilikuwa na uhuru wa kutangaza matokeo bila ya fujo wala vitisho.

“Lakini hata wananchi nao walikuwa wamechoka ndiyo maana wakaamua kufanya maamuzi magumu katika masanduku ya kupigia kura,” alisema Mrema.

Mwenyekiti wa Chauma, Hashimu Rungwe alisema japo ushindi huo umechelewa ukilinganisha na kasi ya watu kudai mabadiliko, imedhihirisha jinsi gani nchi hiyo imeanza kukua kidemokrasia.

Alisema wataendelea kupiga kelele ili Tume ya Uchaguzi (NEC) ibadilishwe na kuwa huru.

Naye katibu mwenezi wa DP, Geras Mwesiga alisema hayo ni matokeo chanya katika mapambano waliyoyafanya kwa muda mrefu kutaka tume huru zinazoweza kutamka ushindi kwa mpinzani.

“Ni ujasiri wa kuigwa na nchi nyingine zijifunze kuwa upinzani si vita wala uadui, bali wao wapo kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi na kuwarekebisha pale mnapokosea,” alisema Mwesiga.

Sifa nyingine kwa Ceni zilitolewa na katibu mkuu wa UPDP, Hamad Mohammed aliyesema mwenyekiti wa tume hiyo ameonyesha dhahiri kuwa hafungamani na chama chochote cha siasa jambo ambalo lilimpa wepesi katika utangazaji wa matokeo.

Matokeo yapingwa

Hata hivyo, hali bado tete baada ya Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa, kusema matokeo hayo hayafanani na yale yaliyohesabiwa na wasimamizi wake.

Taarifa ya kanisa iliyotolewa hii jana haikumtaja mshindi lakini duru za kidiplomasia zinasema kanisa linaamini Fayulu ndiye mshindi

Naye Fayulu alisema timu ya waangalizi 40,000 iliyotumwa na Baraza la Maaskofu la kanisa Katoliki inajua ukweli wa mshindi wa uchaguzi huo.

“Hatuwezi kukubali (kitu kama hiki) mwishoni mwa juhudi za muda mrefu kwamba utashi wa wananchi hauheshimiwi. Wote kwa pamoja tusema hatutaki uchakachuaji wa matokeo,” alisema.

Upinzani umekuwa ukizidi kushinda uchaguzi katika miaka ya karibuni barani Afrika. Miongoni mwao ni Adama Barrow wa Gambia, Nana Akufo-Addo (Ghana), Muhammadu Buhari (Nigeria), na Peter Mutharika wa Malawi

Kwa mara ya kwanza, Congo itashuhudia rais akiachia madaraka kwa amani tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa wakoloni wa Ubelgiji mwaka 1960.

Tshisekedi, mtoto wa mwanasiasa wa zamani wa upinzani, Etienne, atakuwa rais wa sita baada ya Joseph Kabisa, Mobutu Sese Seko, Joseph Kasa-Vubu na Patrice Lumumba.