Washtakiwa watano wa Nemc wapewa dhamana

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapa dhamana washtakiwa watano wa Baraza la Hifadhi ya Mazingira (Nemc) baada ya kupata kibali kutoka Mahakama Kuu kitengo cha Uhujumu Uchumi.

Dar es salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapa dhamana washtakiwa watano wa Baraza la Hifadhi ya Mazingira (Nemc) baada ya kupata kibali kutoka Mahakama Kuu kitengo cha Uhujumu Uchumi.

Washtakiwa hao waliopata dhamana  ni Ofisa wa Mazingira Nemc, Deusdith Katwale (38) na mtaalam wa IT Nemc, Luciana Lawi (33) wote wakazi wa Ubungo Msewe, katibu muhtasi wa Nemc, Edna Lutanjuka (51) mkazi wa Mbezi Beach St Gasper, msaidizi wa ofisa ,Mwaruka Mwaruka (42) na ofisa mazingira Nemc, Lilian Laizer (27) wote  wakazi wa Ukonga Mombasa.

Wafanyakazi hao wamesota rumande tangu Oktoba 31 mwaka huu ambapo walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka sita ya uhujumu uchumi likiwamo la kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari  Makamba katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa mazingira.

Akitoa masharti sita ya dhamana leo Novemba 14 yaliyotolewa na Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando alimtaka kila mshtakiwa kuweka fedha benki kiasi cha Sh. Milioni 13.3 au kuwasilisha mahakamani hapo hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Pia Hakimu Mmbando ametaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika kati yao mmoja awe mwajiriwa wa Serikali, wawe na vitambulisho vya Taifa watakaosaini bodi ya Sh2.5 milioni  kila mtu.

Hakimu Mmbando amewataka washtakiwa hao kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama pamoja na kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani hapo.

Washtakiwa hao pia wametakiwa kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kama watakavyopangiwa.

Baada ya maelezo hayo washtakiwa wote walikamilisha masharti ya dhamana ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Awali Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Jenipher Massue amedai kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika hivyo wanaomba tarehe ya karibu kwani wana nia ya kumuongeza mshtakiwa mwingine.

 

Wakili wa Utetezi Bernard Mbakileki amedai kuwa Mahakama Kuu kitengo cha Uhujumu Uchumi imeridhia mshtakiwa wa pili hadi wa sita kupewa dhamana hivyo wanaiomba Mahakama ya Kisutu iweze kuruhusu utekelezwaji wa amri ya kutoa dhamana. 

Katika hati ya mashtaka washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwamo la kula njama, mawili ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh16O milioni

Mshtakiwa mwenzao ambaye ni ofisa mazingira wa Nemc, Magori Wambura (38) mkazi wa Bombambili hakuwepo mahakamani hivyo ilitolewa hati ya kumkamata ili aje asomewe mashtaka hayo yanayomkabili yeye na wenzake.