Watu 6,099 wapata ajira serikalini kuanzia 2015

Katibu wa Sekretarieti ya ajira, Xavier Daudi

Muktasari:

  • Sekretarieti ya ajira nchini Tanzania imesema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, watu 6,099 wameajiriwa huku 587,746 wakikosa. Kati ya hao 140,000 ndio walioitwa katika usaili

Dar es Salaam. Watanzania 587,746 sawa na asilimia 98.89 walioomba ajira serikalini tangu mwaka 2015 wamekosa ajira hizo,  Sekretarieti ya ajira imebainisha hayo leo Jumatatu Desemba 17, 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa kazi kwa miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, katibu wa sekretarieti hiyo, Xavier Daudi amesema kuanzia Novemba 2015 hadi Desemba 2018, maombi ya kazi yalikuwa  594,300 lakini waliopata ajira ni watu 6,099.

"Tangu Serikali iingie madarakani Sekretarieti ya Ajira imetangaza nafasi za kazi 6,554 kwa ajili ya wizara, idara, wakala, sekretarieti za mikoa, manispaa, halmashauri  na taasisi mbalimbali za elimu," amesema Daudi na kuongeza:

"Jumla ya maombi 594,300 yalipokewa na kufanyiwa kazi, zaidi ya waombaji 140,000 waliitwa kwenye usaili.”

Amesema hadi Desemba 15, 2018 watu 6,099 wamepata ajira na nafasi 455 zilizotangazwa kati ya Novemba na Desemba 2018 mchakato wake unaendelea na utakamilika hivi karibuni.

Hata hivyo, Daudi alisema kuna watumishi wengine 64,814 walioajiriwa kupitia Ofisi ya Rais (Tamisemi) katika kada za afya na walimu.