Watuhumiwa mauaji ya Dk Mvungi waachiwa, wakamatwa tena

Muktasari:

Watu sita wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo wameachiwa huru na Mahakama Kuu na kukamatwa tena, kisha kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu


Dar es Salaam.  Furaha ya kuachiwa huru na Mahakama Kuu ya watu sita wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi ilidumu kwa dakika chache baada ya kujikuta tena mikononi mwa polisi kabla ya kusomewa shtaka jipya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa hao waliachiwa leo Novemba 22, 2018 Mahakama Kuu na Jaji Sam Rumanyika.

Hatua hiyo ni baada ya wakili wa Serikali Nassoro Katuga kuiomba mahakama iwafutie washtakiwa hao shtaka hilo linalowakabili chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) kwa kuwa Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) hana nia ya kuendelea na shtaka hilo dhidi yao.

Kwa mujibu wa sheria kifungu hicho kinatoa mamlaka kwa DPP kumfutia mshtakiwa shtaka linalomkabili wakati wowote, kumkamata na kumfungilia upya mashtaka yanayofanana na yaliyofutwa.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa kesi mpya ya mauaji namba 6, 2018 inayofanana na ile iliyofutwa.

Katika Mahakama ya Kisutu wakili wa Serikali, Lilian Rwetabula aliwataja washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando  kuwa ni Msigwa Matonya(35), Mianda  Mlewa(45), Paulo Mdonondo(35), Longishu Losindo(34), Juma Kangungu(34) na John Mayunga(60).

Katika kesi hiyo mpya ya mauaji namba 6, 2018,  washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Novemba 3, 2013 walifanya kosa hilo la mauaji ya kukusudia  kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo  ya tukio katika eneo la Msakuzi Kiswegere  lililopo Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk Mvungi.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Hata hivyo, pamoja na hayo mshtakiwa Longishu alinyoosha mkono mahakamani hapo na aliporuhusiwa aliiambia Mahakama kuwa kesi hiyo siyo mpya ni ya mwaka 2013 imepewa tu namba mpya.

Kwa upande wa mshtakiwa Mayunga yeye aliomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa muda muafaka kwa sababu hakuna jipya kila kitu kilikwishasomwa.

Hata hivyo muda mfupi baadaye washtakiwa hao walisomewa shtaka hilo jipya katika Mahakama ya Kisutu.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Desemba 6, mwaka huu na washtakiwa kupelekwa rumande.

Soma zaidi:

Mei 4,2017

Washtakiwa hao, washtakiwa hao walisomewa maelezo ya mashahidi wa tukio, Maelezo yao wenyewe  na vielelezo (Committal proceedings) mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa Mashahidi 30 wa upande wa mashtaka wanatarajiwa kutoa ushahidi Mahakama Kuu katika kesi hiyo ya mauaji .

Hayo yalielezwa na Wakili wa Serikali, Patrick Mwita.