Wazazi wa mtoto aliyefariki baada ya kukeketwa kusakwa

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima 

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amemwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Serengeti kuwasaka wazazi wa mtoto anayedaiwa kufariki dunia baada ya kukeketwa na maiti yake kutupwa


Serengeti. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amemwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Serengeti kuwasaka wazazi wa mtoto anayedaiwa kufariki dunia baada ya kukeketwa na maiti yake kutupwa.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 18, 2018 katika kikao cha baraza la madiwani, Malima amesema lazima watuhumiwa wakamatwe na kutaka wazazi hao nao wasakwe.

Malima amebainisha kuwa Serikali haiwezi kukubali watu kufanya mambo ya hovyo na yanayovunja haki za binadamu na hatua hazichukuliwi.

"Hili ni agizo naomba muwatafute hao wazazi na waliohusika wote wakamatwe hatuwezi kuchezewa na watu kwa kuvunja sheria za nchi," amesema.

Ameomba madiwani kushirikiana na vyombo vya dola kuwakamata wahusika wote wanaoendesha ukeketaji katika mkoa wa Mara.