Waziri Kairuki alivyopona kuutema uwaziri

Angellah Kairuki


Muktasari:

Angellah Kairuki ni mbunge wa viti maalumu tangu mwaka 2010 na alizaliwa Septemba 10, 1976. Aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi pia Wizara ya Katiba na Sheria.



Dar es Salaam. Kama kuna waziri ana bahati na Rais John Magufuli, basi ni waziri mpya wa uwekezaji, Angellah Kairuki.

Kairuki amehamishiwa wizara hiyo iliyoondolewa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara baada ya Rais kubaini udhaifu katika utendaji na kuusema hadharani wakati akimwapisha aliyekuwa naibu wake, Dotto Biteko kuwa Waziri wa Madini, akimuonya naye kuwa akiboronga ataondolewa.

Akiwa ameshawatema mawaziri tisa katika miaka mitatu tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amesisitiza kuwa hatajali kubadilisha mawaziri hata kama ni kila siku.

Mawaiziri walioenguliwa tangu Rais Magufuli aingie madarakni ni pamoja na Charles Kitwanga (Mambo ya Ndani), Nape Nnauye (Habari), Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani), Dk Charles Tizeba (Kilimo), Charles Mwijage (Viwanda), Gerson Lwenge (Maji na Umwagiliaji) na Profesa Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii).

Kati yao, ni Nape, Maghembe na Lwenge pekee ambao Rais hakueleza udhaifu wa wizara zao hadharani.

Wakati mawaziri wenzake ambao udhaifu wa wizara zao ulianikwa hadharani na pia kuenguliwa, kwa mara ya pili Kairuki ameendelea na uwaziri.

Hii inakuwa wizara ya tatu kwa Kairuki katika miaka mitatu. Alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utumizi na Utawala Bora) kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Madini baada ya kutenganishwa na Nishati.

“Kairuki ana uwezo mkubwa kiutendaji, ila hajapangiwa nafasi inayomfaa,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alipoulizwa kuhusu hali hiyo.

“Wizara ya Madini kama zilivyo wizara za Maliasili na Utalii na (ya) Mambo ya Ndani zina mambo mengi. Waziri Kairuki ni mwanasheria mzuri na alifanya vizuri hata wakati wa Bunge la Katiba. Wizara aliyokuwepo ilikuwa technical (kiufundi) zaidi.”

Hata hivyo, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha cha Iringa alisema tatizo si utendaji wa mtu mmoja mmoja bali ni la kisera za kitaifa.

“Hayo mambo ya kiutendaji yapo na ni makosa, lakini bila kuwa na sera nzuri za kitaifa, sekta ya madini itaendelea kuwa tatizo,” alisema.

Ni katika Wizara ya Madini ambako amekumbana na matatizo hayo. Mara ya kwanza ni wakati wizara hiyo iliposhindwa kuunda kanuni za sheria ya madini na hivyo kushindwa kufanya kazi, hali iliyomlazimisha Rais kumteua Biteko kuongeza nguvu kwenye wizara hiyo mpya na hivyo kuwa na manaibu wawili.

Akizungumza wakati wa kumwapisha Biteko Januari 6 mwaka jana, Rais alisema wizara hiyo haifanyi kazi vizuri.

“Unajua nikizungumza kwa kupamba, nitakuwa mnafiki,” alisema kabla ya kuchambua udhaifu wa wizara hiyo.

Alisema tangu Bunge lilipopitisha mabadiliko ya Sheria ya Madini Na. 7 ya 2017 na yeye mwenyewe kuitia saini, waziri husika hakutia saini kanuni zake kwa miezi saba.

“Waziri yupo, Naibu Waziri yupo, kamishna ambaye ndiye mshauri mkuu wa waziri yupo, wakurugenzi wapo,” alisema Rais Magufuli.

“Unaweza kusema tuna matatizo makubwa sisi kama Serikali. Kwa sababu kama zile regulations (kanuni) hazijasainiwa, mnategemea nini? Kwa kuanzia mwezi wa saba hawakusaini, wa nane, wa tisa, wa 10, 11 wa 12.”

“Sisi Watanzania saa nyingine baadhi ya watendaji serikalini they are not serious (hawako makini). Ninasema hii nikiwa na uchungu mkubwa, kwamba baadhi ya ninaowateua bado hawajanielewa ninataka nini na inawezekana bado hawajaelewa Bunge linataka nini, Watanzania wanataka nini,” alisema.

Rais Magufuli alisema kutokana na udhaifu huo aliamua kumwongezea Biteko na kuifanya wizara hiyo kuwa na manaibu waziri mawili pamoja na Stanslaus Nyongo.

Katika mabadiliko mapya, wizara hiyo itabakia na naibu mmoja.

Jumanne, Rais Magufuli pia alichambua udhaifu wa Wizara ya Madini, ambayo sasa ina zaidi ya mwaka tangu ianzishwe.

Wakati akimwapisha Biteko kuwa waziri mpya wa Madini, alishangaa Tanzania kutoongoza katika nchi za Afrika zinazouza madini licha ya kuchimba dhahabu nyingi.

Pia alisema hakuna vituo vya kununulia madini, jambo linalosababisha wachimbaji kutafuta mbinu nyingine.

Alisema Serikali inatetea wachimbaji wadogo, lakini haijui wanauzia wapi madini wanayopata, kitu ambacho kinasababisha yapotee na Serikali isinufaike.