Waziri asema Sh40bilioni zimetumika kununua korosho

Muktasari:

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda amesema zaidi Sh40 bilioni zimetumika kununua korosho kwa wakulima 40,000 kati ya Sh528 bilioni zinazotarajiwa kununua tani 160,000 zilizopo katika maghala


Dar es Salaam.  Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda amesema zaidi Sh40 bilioni zimetumika kununua korosho kwa wakulima 40,000 kati ya Sh528 bilioni zinazotarajiwa kununua tani 160,000 zilizopo katika maghala.

Kakunda ameyasema hayo leo Jumatano Desemba  5, 2018  jijini Dar es Salaam alipotembelea maonyesho ya bidhaa za viwandani ambayo yatafunguliwa rasmi kesho katika viwanja vya Sabasaba jijini humo.

Kakunda amesema tani 275,000 za korosho zinatarajiwa kuvunwa msimu huu na mpaka sasa tayari wakulima wamevuna na kuuza tani 160,000 na tani nyingine 100,000 zikitarajiwa kuvunwa mwezi huu.

"Zoezi la kuwalipa wakulima linakwenda vizuri mpaka jana zaidi ya Sh40 bilioni zilikuwa zimetumika. Changamoto tunayokabiliana nayo ni upungufu wa mashine za kubangulia korosho, kwa hiyo tumepanga kuhifadhi korosho wakati tukisubiri maelekezo mengine ya viongozi wetu," amesema Kakunda.

Waziri huyo amesema wanaendelea kupambana na wafanyabiashara wanaowadhulumu wakulima kwa kununua mazao yao yakiwa bado shambani. Amesema mpaka sasa watu 20 wamefikishwa mahakamani kwa kosa hilo na hukumu zao zimetolewa.

"Wale waliopanga kuwadhulumu wakulima tunawashughulikia. Kila mkulima anayeleta korosho zake tunakwenda kuangalia shamba lake, tumewadhibiti wale wanaoleta korosho wanazowadhulumu wakulima," amesema.