Wenye shule binafsi wamjibu Waitara wanafunzi kurudi nyumbani

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara

Muktasari:

Baadhi ya shule zilizoshutumiwa kutofuata sheria za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kurudisha wanafunzi nyumbani kwa kutolipa ada wametoa ufafanuzi kuwa wanafanya hivyo kutokana na kutokuwa na chanzo cha gharama za uendeshaji zaidi ya ada.

 


Dar es Salaam.  Siku moja baada ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara kupiga marufuku wanafunzi wa shule binafsi ambao hawajamaliza ada kusimamishwa au kufukuzwa shule, baadhi ya shule zilizotajwa kukiuka agizo hilo, zimetoa ufafanuzi.

Akizungumza na vyombo vya habari jana Alhamisi, Waitara alizitaka shule kutowarudisha wanafunzi nyumbani wanaposhindwa kulipa ada na kutokaririsha madarasa huku akizitaja baadhi ya shule kuhusika na tuhuma hizo.

Miongoni mwa shule zilizotajwa ni pamoja na Sekondari ya Green City iliyopo mkoani Morogoro na Sekondari ya Taqwa ya mjini Mwanza.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 11,2019 kwa sharti la kutotaja jina lake, meneja wa Shule ya Green City amesema hawajawahi kumfukuza mwanafunzi wala kumrudisha nyumbani kwa sababu ya ufaulu.

Amesema waliokaririshwa madarasa ni kutokana na makubaliano ya wazazi baada ya kujadiliana nao kuhusu maendeleo ya watoto wao.

“Hakuna mwanafunzi aliyerudishwa au kukaririshwa darasa kwa ajili ya wastani kiholela, hakuna, waliokaririshwa ni kwa mujibu wa waraka namba mbili wa mwaka 2018 ambapo wazazi waliandika barua na tunazo hapa shuleni, ”amesema meneja huyo.

Kuhusu kurudisha wanafunzi kwa kutolipa ada amekanusha akidai maelezo yaliyotolewa ni ya uongo.

“Maelezo yote uliyopewa ni ya uongo, hatujawahi kufanya hivyo.”

Kwa upande wa Mbaraka Mohamed meneja shule za Sekondari Taqwa zilizopo mjini Mwanza amesema hawajawahi kumrudisha mwanafunzi bila kuwasiliana na wazazi.

“Tunajua hali za wazazi na tuna utaratibu hapa shuleni, mzazi akija tunazungumza naye na tunampa utaratibu wa kulipa ada na risiti aliyolipa mara ya mwisho inatolewa kopi na kuandikwa nyuma ili wanapokuja wakaguzi mwanafunzi hatolewi darasani wala kurudishwa nyumbani, anakuwa salama kwa sababu wazazi wametoa taarifa,” amesema Mohamed.

Amesema wanakubaliana na wazo la kutowarudisha wanafunzi wasiolipa ada, lakini wanaomba wapewe suluhisho kwa sababu hawana chanzo kingine cha fedha kuendeshea shule zao.

 “Hatuna chanzo kingine, kuendesha shule kunahitaji maji, umeme, mishahara ya walimu na mahitaji mengine muhimu. Kama huna fedha, hivi vyote haviwezi kufanyika, tunawaita wazazi shule zinapofungwa na tunawapa barua wanafunzi, lakini hawaji tukae nao tujadili kwa pamoja.”

Amesema: “Kwa mfano, hapa kwetu ada ni nafuu sana, shule ya awali wanalipa (Sh) 400,000 kwa mwaka, ya msingi wanalipa 500,000 kwa mwaka na sekondari wanalipa 750,000 kwa mwaka na wanalipa kwa awamu lakini mwanafunzi anakaa hadi mwezi hajalipa anahudumiwa na nini huyu.”

Amesema mwanafunzi anahudhuria masomo hadi wiki moja bila taarifa yoyote kutoka kwa mzazi, hivyo wanalazimika kumrudisha na wakifanya hivyo anakwenda na wanajadiliana pamoja.

Kuhusu kuwarudisha wanafunzi nyumbani kwa ufaulu, Mohamed amesema kuwa alama za Serikali ni asilimia 30, lakini wanafunzi wakipata asilimia 25 ikiwa na maana chini hata ya alama zinazowaongoza, ni lazima wazazi wajadiliane na walimu nini cha kufanya.

“Ukiwaita wazazi hawaji, unatumia njia rahisi ni kumrudisha nyumbani mwanafunzi. Ukifanya hivyo wanakuja nao na kujadili tufanye nini,” amesema.