Wizara yazungumzia waraka wa kukariri, kuhamisha wanafunzi

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk Leonard Akwilapo

Muktasari:

  • Wizara ya Elimu imesema itatoa waraka unaoelekeza utaratibu wa kukariri ama kuhamisha wanafunzi kabla ya Januari 2019

Dodoma. Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk Leonard Akwilapo amesema waraka unaelekeza utaratibu wa kukariri na kuhamisha wanafunzi utatolewa kabla ya Januari 2019.

Dk Akwilapo ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 10, 2018 katika mkutano wa wakuu wa shule za Sekondari za makanisa jijini hapa.

Amesema mwaka mpya wa masomo unakaribia kuanza inailazimu wizara hiyo kutoa mwongozo ili kuwa na maridhiano kati ya wanafunzi na wazazi.

“Ofisi ya kamishna wa elimu imeshaandaa mwongozo huo kwa kushirikiana na wamiliki wa shule na zisizo za Serikali. Natarajia mtapata huo mwongozo kabla hamjaondoka hapa Dodoma hiyo siku ya Jumatano," amesema.

Awali Mkurugenzi wa Huduma za Elimu wa Tume ya Kikiristo ya Huduma za Jamii (CSSC), Petro Pamba amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni upimaji wa umahiri wa wanafunzi kwa kuzingatia umahiri wa kutoka darasa moja kwenda jingine.