Wizara zajifungia kujadili viwanda

Muktasari:

  • Mawaziri hao katika kikao kinachoongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama wanafanyia kazi maagizo ya Serikali ya kuhakikisha sekta wanazoziongoza zinatoa mchango katika ujenzi wa viwanda nchini.

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama ameongoza kikao cha mawaziri na watendaji wakuu wa wizara kuandaa mpango mkakati wa ujenzi wa viwanda.

Kikao hicho kilichofanyika jana jijini hapa, kilikuwa kinafanyia kazi maagizo ya Serikali kwa mawaziri kuhakikisha sekta wanazoziongoza zinatoa mchango katika ujenzi wa viwanda kwa kufanya mapitio ya kanuni, sera na sheria.

“Niwaombeni wote mliopo hapa kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu kwa kutekeleza programu hii ya ujenzi wa uchumi wa viwanda ikiwa ni njia ya kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatumika kwa manufaa ya nchi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania,” alisema Mhagama.

Programu hiyo imejikita katika kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji nchini kwa lengo la kuvutia sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi.

“Programu hii imelenga kukuza uchumi na ujenzi wa viwanda kwa kufuata misingi na kanuni za kibiashara zinazokubalika kimataifa, kuhakikisha viwanda vinakuwa chachu ya maendeleo nchini,” alisema Mhagama.

Kikao hicho kilihudhuriwa na mawaziri, Profesa Makame Mbarawa (Maji na Umwagiliaji); Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango); Isaack Kamwelwe (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano); Dk Medard Kalemani (Nishati) na Joseph Kakunda wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Wengine ni Naibu Waziri wa Tamisemi; Mwita Waitara wenzake Stanslaus Nyongo (Madini) na Omary Mgumba na Innocent Bashungwa wa Kilimo na katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Faustine Kamuzora.

Akizungumzia programu hiyo, Profesa Kamuzora alisema, “Kila wizara iandae mpango mkakati wa namna bora ya kufanikisha utekelezaji kwa kushauriana na wadau wa sekta binafsi ambao ni wadau muhimu.”

Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Godfrey Mwambe alisema

“Tunataka kuona viwanda vinakuwa soko la mazao yanayozalishwa na wakulima.”