UCHOKOZI WA EDO: Yalianza mafao yetu, sasa wimbo wa Nyegezi

EdoKumwembe

Namuweka kando Bernard Membe, labda nitaongelea kesho kitu kidogo kuhusu mtego aliowaingiza watu kwa sasa, halafu mwenyewe amebaki anacheka. Leo siuingii mtego wake.

Wakati Membe akitamba kule Twitter, macho yangu yalikuwa katika mtandao wa Instagram. Wabunge wetu walikuwa wakitamba huko. Wameshinda baadhi ya mechi zao za wabunge wa Afrika Mashariki kule Burundi.

Baada ya kushinda juzi wakaanza kukatika wakishangilia kwa kucheza wimbo wa nyegezi. Nilicheka. Ndio, ni wimbo uliofungiwa na BASATA. Wimbo wa vijana wasumbufu kutoka kundi linalojiita Wasafi. Linaloongozwa na Diamond Platinumz. Mmoja kati ya watu maarufu zaidi nchini.

Tulisikia ikielezwa kuwa wimbo huo ni marufuku kuchezwa redioni na maeneo mbalimbali. BASATA kama wangekwenda na kauli ya Agrey Mwanri basi ingekuwa wimbo huo ukipigwa ni marufu hata ‘kujikuna’.

BASATA wanafanya kazi yao kwelikweli lakini wakati mwingine hutupiwa lawama na wabunge wakiwa Dodoma. Kisa? Hudai baraza hilo kutokuwa wakali katika kuchunga maadili ya wasanii nchini. Leo wameufungia wimbo lakini watunga sheria hao wanakatika. Inachekesha kwelikweli.

Siwashangai sana. hata kwenye mafao yetu ya uzeeni hadithi ni hiyo hiyo. Wao mafao yao yametulia kibindoni na hayana shaka. Baada ya miaka mitano wanapokea chao wanarudi majimboni. Katika lugha rahisi wao wamejitengenezea utaratibu wa ‘kila mtu afe na chake’.

Sisi wengine mafanikio yetu wametupangia tupokee robo robo. Tutafika kweli? Muda pekee ambao wabunge wanatupenda kuliko wanavyojipenda ni wakati wa kwenda chini ya miembe kuweka tiki katika alama ya ‘NDIYO’ ndani ya karatasi ya kura. Zaidi ya hapo inaonekana tunachezeana akili tu.

Kwa nini suala la mafao yetu tusishauariane katika kufikia mwafaka? Inawezekana vipi fedha yangu ikatafutiwe ufumbuzi wa matumizi na mtu mwingine? Hata kama imechangiwa na pande zote mbili bado ilihitaji majadiliano na makubaliano.

Hata hivyo, tunaweka kichwa chini kama kawaida yetu tunawatazama wanavyocheza Nyegezi. Wimbo ambao kwetu ni marufuku lakini kwao ni ruksa. Sawa sisi wanyonge. Tutakutana Twenti Twenti.