Zitto: 2019 ni mwaka wa kudai demokrasia

Muktasari:

Zitto Kabwe, kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema 2019 ni mwaka wa vyama sita vya upinzani nchini Tanzania kudai demokrasia

Unguja.  Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo,  Zitto Zubeir Kabwe amesema  vyama sita vya upinzani nchini Tanzania vilivyotoa tamko la pamoja leo Jumanne Desemba 18, 2019 vimeazimia kuutumia mwaka 2019 kudai demokrasia.

Akizungumza na Mwananchi baada ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kumaliza kusoma tamko hilo, Zitto amesema Tanzania kuna ukiukwaji wa demokrasia, kubainisha kuwa bila kupambana hali ya vyama vya upinzani itakuwa ngumu zaidi.

Amesema kila mmoja anapaswa kupambana na hali ya mgogoro wa kidemokrasia, lazima wajitoe kupigania jambo hilo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema waliyokubaliana Zanzibar yatatekelezwa kwa vitendo kwa sababu ni maelekezo yaliyopo hata katika Katiba ya nchi hiyo.

Amesema kutokana na ukiukwaji wa demokrasia ni lazima kila mtu apambane kudai haki vinginevyo mambo makubwa zaidi yanaweza kutokea.

Leo vyama hivyo sita vilivyofanya mkutano wa faragha wa siku mbili visiwani Zanzibar tangu jana, vimetoka maamuzi mawili mazito.

Katika mkutano huo ulioratibiwa na CUF, vimeazimia kuanza kufanya mikutano ya hadhara kwa kuwa ni haki yao kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.

Pia, wametangaza rasmi kwamba wanasiasa wote waliopo jela kwa tuhuma za kisiasa hao ni ‘Wafungwa wa kisiasa’ na kuanzia sasa wataitangazia dunia hivyo.

Tamko hilo limesainiwa na Maalim Seif, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia; mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi; naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu; mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Vyama hivyo vimetoa uamuzi huo wakati Serikali ya Tanzania ikiwa imepiga marufuku mikutano yote ya kisiasa ya hadhara mpaka mwaka 2020 isipokuwa kwa wabunge walioshinda uchaguzi ambao wameruhusiwa kufanya mikutano kwenye majimbo yao tu.

Miongoni mwa viongozi wa upinzani walio mahabusu ni pamoja na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko ambaye pia ni mbunge wa Tarime Mjini.