Zitto: Mswada utaondoa mfumo wa vyama vingi

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe

Muktasari:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema muswada wa marekebisho wa sheria ya vyama vya siasa utaondoa mfumo wa vyama vingi

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema muswada wa marekebisho wa sheria ya vyama vya siasa ukiwa sheria mfumo wa vyama vingi vya siasa utaondoka.

Zitto amesema hayo leo  wakati wa mkutano uliovikutanishwa vyama 15 vya siasa vya upinzani kupinga muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa uliosomwa bungeni Novemba 16 mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano huo,  Kabwe amesema wapo watu waliopambana ili kuhakikisha demokrasia ya mfumo wa vyama vingi unakuwepo nchini.

“Wengine walikuwa ni wanafunzi walijitolea kuhakikisha demokrasia hiyo inakuwapo kikamilifu hivyo na sisi tunaahidi kuwa tutaulinda kikamilifu ili kuhakikisha haupitishwi kuwa sheria,” amesema Zitto

Amesema japo kuwa muswada huo bado haujapitishwa lakini utekelezaji wake kupitia chama tawala umeanza kuonekana na unalenga kudhoofisha na kuua vyama vingine vya siasa.

“Tutasimama kikamilifu kuhakikisha hilo halitokei japo kutakuwa na chokochoko nyingi zinazolenga kutugawa lakini tutasimama imara,” amesema Kabwe.