Zitto atumia dakika 240 Takukuru

Muktasari:

2.9 milioni ni Kiwango cha tani za chuma ambazo zinategemewa kuzalishwa na mgodi wa Liganga.

600 ni Idadi ya megawati za umeme zina-zotarajiwa kuzalishwa kwa kutumia makaa ya mawe ya mgodi wa Mchu-chuma; megawati 350 zinatarajiwa kuingizwa katika gridi ya Taifa na zilizobaki kutumika katika mgodi kwa ajili ya kuchenjua na kuzalisha chuma cha pua.

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe jana alitumia takriban saa nne kuwasilisha Takukuru ushahidi wake kuhusu madai ya rushwa ilivyozingira mradi wa Liganga na Mchuchuma, lakini anahofia kama taasisi hiyo itafanyia kazi vielelezo vyake.

Zitto anakuwa mwanasiasa wa pili kuwasilisha vielelezo vyake vya tuhuma za rushwa dhidi ya viongozi au watendaji wa Serikali, baada ya mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari kufanya hivyo mwaka jana, lakini Takukuru ikaliacha suala hilo kwa madai kuwa amegeuza kuwa la kisiasa.

Zitto anafuata mkondo huo baada ya kuanzisha sakata hilo kwenye mitandao ya kijamii, akidai kuwa kampuni tatu za China, Uturuki na Urusi zimehonga viongozi wa Serikali ili wakwamishe utekelezaji wa mradi huo kwa lengo la kuhakikisha nchi hizo zinapata soko la chuma.

Kauli hiyo ilimfanya mbunge huyo wa Kigoma Mjini kuitwa na Takukuru kwa ajili ya kushirikiana katika kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha ushahidi. Alianza kazi hiyo juzi.

Kiongozi huyo alitumia zaidi ya saa nne kukamilisha ushahidi na kutoa vielelezo alivyodai kuwa ni nyaraka mbalimbali za Serikali pamoja na hati ya kiapo baada ya juzi kushindwa kumaliza kutokana na kuwa na majukumu mengine.

“Azma yangu ni kuona mradi huu unatekelezwa kwa sababu una faida kubwa kwa Taifa,” alisema Zitto baada ya kutoka nje ya ofisi za Takukuru zilizopo Upanga jijini hapa.

“Nimehojiwa tena leo (jana) kati ya saa 3:00 hadi saa hizi, saa 7:00 na nimetoa vielelezo ambavyo nimetakiwa kuwapatia na pia nimeomba kuwasilisha hati ya kiapo ambayo ina maelezo ya ziada na nyaraka za Serikali ambazo zinaenda kuthibitisha hizo hisia zangu.”

‘Takukuru wameingia mtegoni’

Hata hivyo, Zitto alisema ana shaka kama Takukuru itafanyia kazi mchango wake.

“Nimewapatia nyaraka na nitawapatia nyaraka nyingine lakini nimewaonyesha mashaka yangu kwamba hawatafanya uchunguzi,” alisema.

Alisema baadhi ya maamuzi ya kupitisha mradi huo yanawahusu viongozi wa juu wa Serikali.

“Nimewaambia Takukuru kwamba naamini jambo hili mnalifanya lakini hamtafika kokote. Lakini mimi naliweka kwenye rekodi ili ionekane kwamba mlinitaka nitolee maelezo na nilitoa,” alisema.

“Kwa hiyo Takukuru wameingia kwenye mtego ambao itakuwa vigumu sana kutoka.”

Alisema mradi huo umeshindwa kufanyika tangu mwaka 2011 kutokana na kile alichokiita kuwa ni “hila” za baadhi ya watendaji wa Serikali pamoja na kampuni zinazofaidika na biashara hiyo.

Alisema mradi huo ni muhimu kwa nchi endapo utatekelezwa, akisema ulipangwa kuzalisha tani milioni 3 za chuma kwa mwaka, ambazo zingeliingizia Taifa jumla ya Sh12 bilioni kwa mwaka.

Mbunge huyo alisema kiasi hicho cha fedha kingewezesha kuendesha mambo mbalimbali kwa kutumia fedha za ndani, kama ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR).

“Kwangu mimi huu ni mradi muhimu sana. Ukiachana na ajira zaidi ya 35,000, ungesaidia ujenzi wa viwanda mama, ujenzi wa reli ambao tungeweza kutumia chuma chetu wenyewe,” alisema.

Alisema mbali na chuma, mradi huo utasaidia kuzalisha madini aina ya vanadium ambayo yakiuzwa nje yatasaidia kupata fedha za kigeni na kupunguza gharama mbalimbali kwenye matumizi ikiwamo uagizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

“Hakuna makinikia kwenye chuma, kila kitu lazima kiongezewe thamani hapa nchini kabla ya kusafirishwa. Kwa hiyo mtu yeyote mwenye mapenzi ya dhati kwa nchi kikubwa ambacho angekifanya ni kuanza kutekeleza mradi huu.”