Naibu Katibu Mkuu ataka fedha za miradi zilizobadilishiwa matumizi kurejeshwe

Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tamisemi Tixon Nzunda

Muktasari:

  • Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tamisemi Tixon Nzunda ametoa mwezi mmoja kwa  baadhi ya halmashauri za mikoa ya Kigoma, Shinyanga na Mara zilizobadilisha matumizi ya fedha za mradi wa kukuza ubora wa elimu ya msingi (EQUIP) Tanzania na kutaka fedha hizo zirejeshwe. Fedha hizo zinakadiliwa kuwa zaidi ya Sh500 milioni

Morogoro.  Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tamisemi Tixon Nzunda ametoa mwezi mmoja kwa  halmashauri zilizobadilisha matumizi ya fedha za mradi wa kukuza ubora wa elimu ya msingi (EQUIP) Tanzania na kutaka fedha hizo zirejeshwe. 

Nzunda ametoa agizo hilo jana jioni Desemba 8 wakati wa kikao chake na wakurugenzi, maofisa elimu  wa mikoa  na wilaya  na maofisa mipango  wa halmashauri  za mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Kigoma, Simiyu, Lindi, Mara, Tabora, Singida na Katavi ambapo walijadili namna bora ya kutekeleza mradi huo.

Amesema baadhi ya halmashauri ambazo zimebadilisha fedha za mradi huo zinazokadiriwa kuwa Sh500 milioni zipo katika Mkoa wa Kigoma, Shinyanga na Mara ambapo alizitaka kurejesha fedha hizo mapema ili zitumike kukamilisha mradi uliokusudiwa.

“Serikali ya awamu ya tano kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kimataifa imejielekeza katika kuboresha kiwango cha elimu hivyo hakuna fedha yoyote ya mradi wa elimu itakayoliwa,” amesema Nzunda.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  Dk Avemaria Semagafu ambaye alikuwapo katika kikao hicho aliwaonya maofisa elimu wenye tabia ya kuchagua wanafunzi wasiokuwa na sifa kujiunga na kidato cha kwanza na hivyo kusababisha msongamano kwenye madarasa. 

Amesema imekuwa ni tabia ya baadhi ya maofisa elimu kushindana kufaulisha wanafunzi hasa wa darasa la saba jambo ambalo linasababisha kuwapo kwa matukio ya udanganyifu wa mitihani na mengine yanaporomosha kiwango cha elimu. 

Mratibu wa mradi huo wa EQUIP Tanzania,  Steven Myamba amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa tisa na unalenga kutoa mafunzo kwa walimu na kuboresha miundombinu mbinu ya kufundishia na kujifunza.