Kituo cha kupoza umeme chazinduliwa Dar

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu akiwasha mtambo wa kupoza umeme katika kituo kipya cha kupoza umeme kilichopo Mbagala jijini Dar es Salaam

Muktasari:

Ni baada kuzinduliwa kwa mtambo wenye uwezo wa kupoza megawati 40


Dar es Salaam. Changamoto ya upatikanaji wa umeme katika jiji la Dar es Salaam imeendelea kupatiwa ufumbuzi baada ya kuwashwa kwa mtambo kwenye kituo kipya cha kupozea umeme kilichopo Mbagala.

Mtambo huo wenye uwezo wa kupoza megawati 40 umetajwa kuwa suluhisho la kukatika mara kwa mara kwa nishati hiyo katika maeneo ya Mbagala, Tandika, Mkuranga na Kigamboni.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasha mtambo huo leo Februari 22, 2018, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema tatizo la umeme linakwenda kuwa historia.

Amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni utekelezaji wa mradi mkubwa unaohusisha vituo 19 katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro.

Amesema awali kituo kilichokuwepo kilikuwa na mzigo mkubwa ikizingatiwa maeneo hayo yana mahitaji makubwa ikiwemo viwanda.

"Serikali imeendelea kuifanyia kazi changamoto ya umeme na ninachoweza kuwaambia wakazi wa Mbagala sasa hivi mambo safi nishati hii itakuwa ya uhakika,” amesema.

"Niwaombe radhi wakazi wa maeneo hayo kutokana na changamoto hiyo iliyowakabili kwa muda mrefu, tulikuwa tunaitafutia ufumbuzi na sasa kila kitu kitakwenda sawa.”

Amewataka wenye viwanda kutumia fursa hiyo ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kuongeza uzalishaji maradufu.

Aidha Waziri Mgalu amewataka wakazi wa maeneo ya jirani na kituo hicho kulinda miundombinu ya umeme ili kuepuka kulitia hasara shirika la umeme Tanesco.

Amesema kuiba au kuharibu miundombinu ya umeme inahesabiwa kama uhujumu uchumi na wahusika hawatakiwi kufumbiwa macho.

Amezitaka pia kamati za ulinzi na usalama katika mitaa yote nchini kuhakikisha zinalinda miundombinu hiyo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watakaobainika kuhujumu.

Kauli hiyo ya naibu waziri ameitoa baada ya Kaimu Meneja mwandamizi miradi wa Tanesco, Mhandisi Emmanuel Marinabona kueleza kuwa licha ya upya wa kituo hicho tayari watu wameshaanza kuharibu miundombinu.