Wednesday, January 11, 2017

Kituo cha wanaokimbia kukeketwa chaelemewa

 

By Waitara Meng’anyi, Mwananchi wmeng’anyi@mwananchi.co.tz

Tarime. Kituo kinachotumika kuwatunza wasichana wanaokimbia kukeketwa cha Association for Termination of Female Genital Mutilation (ATFGM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, kimelalamikia kuelemewa na mzigo.

Mratibu wa kituo hicho, Valerian Mgani amesema hali hiyo inatokana na familia za wasichana 80 waliokimbia kukeketwa kukataa kuwapokea.

Valerian amesema wamefanya juhudi mbalimbali za kuwashawishi wazazi na wale wa mabinti hao, lakini zimeshindikana tangu Januari 3

Wasichana hao walikimbia kukeketwa mwishoni mwa mwaka jana kutoka kata za Susuni, Mwema na Komaswa.

“Hivi sasa kituo kimeelemewa na mzigo wa kuwatunza wasichana hawa kutokana na bajeti ya kuwahudumia kuisha, walipaswa kurejea nyumbani kwao kuendelea na masomo baada ya msimu wa ukeketaji kufikia mwisho,” amesema Mgani.

Amefafanua kuwa kitendo cha watoto hao kukataliwa kimesababisha washindwe kuendelea na masomo baada ya shule za msingi na sekondari kufunguliwa juzi.

Mkurugenzi wa ATFGM, Sista Stella Mgaya amesema hiyo siyo mara ya kwanza familia kukataa kuwapokea watoto wao waliokimbia kukeketwa na tohara isiyo salama kwa wavulana.

Hata hivyo, Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Sylvester amesema suala hilo linaweza kushughulikiwa na mamlaka za juu na kushauri atafutwe Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo, Apoo Tindwa.

-->