Kitwanga amtaka Dk Mpango kung’oka

Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Ametoa kauli hiyo leo jioni Alhamisi Mei 24, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2018/19.


Dodoma. Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amesema kama Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango anadai  hana fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ni vyema akajiondoa katika wadhifa huo.

Kitwanga ambaye ni mbunge wa Misungwi (CCM) ametoa kauli hiyo leo jioni Alhamisi Mei 24, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2018/19.

Mbunge huyo ameishauri Serikali kuangalia mipango ya kuanzisha miradi mikubwa ya kuzalisha umeme, kuachana na miradi midogo.

“Hivi kwanini unakosa fedha? Kama ni waziri wa fedha halafu unasema

hakuna fedha ondoka hapo,” amesema.

Amesema miradi midogo ina gharama kubwa za uendeshaji ikiwemo kuwalipa mishahara watumishi wanaohudumia katika vituo hivyo na kumshauri  Waziri wa Nishati,  Dk Medard Kalemani kuja na mpango wa kuzalisha umeme wa Megawati 5,000 kwa kutumia makaa ya mawe.

“Wazungu wanasema uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe unachafua hali ya hewa lakini wao wanazalisha umeme kwa kutumia makaa hayo kwa sababu teknolojia imebadilika,” amesema.

“Duniani kote umeme wa bei nafuu ni unaozalishwa na maji  ama

Makaa.”