Kitwanga awashukia watendaji

Muktasari:

  • Mbunge ataka kama wameshindwa kukusanya mapato wampe kazi hiyo

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, limewapa muda wa siku 30 watendaji kushughulikia suala la makusanyo ya mapato ya ndani na utekelezaji wa mradi wa maji katika kijiji cha Fela uliokwama tangu 2013.

Azimio hilo lilipitishwa na baraza hilo wakati wa kikao kilichofanyika mjini Misungwi juzi, baada ya kubainika kuwa hadi Desemba 2017 halmashauri hiyo imekusanya Sh734.9 milioni pekee kati ya malengo ya kukusanya Sh2.06 bilioni.

Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga ndiye alikuwa mwiba mchungu kwa watendaji kwa kudai maelezo sababu ya ukusanyaji mapato kusuasua, hali inayokwamisha utekelezaji wa miradi.

Alitaja mwalo la Mbarika ambako vitabu vya halmashauri vinaonyesha hakuna mapato yanayokusanywa, lakini hivi karibuni kamati ya uchumi na mipango ilipotembelea eneo hilo ilifanikiwa kukusanya Sh15,000 kwa muda mfupi, hali inayodhihirisha ulegevu kwenye ukusanyaji.

Kuhusu mradi wa maji wa Fella ambao utekelezaji wake ulianza Juni 2013 na kutakiwa kukamilika Desemba mwaka huo, baraza limempa siku 30 mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Eliud Mwaiteleke kuhakikisha unakamilika na kutoa maji au uwekwe chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mradi huo ambao tayari umegharimu zaidi ya Sh644 milioni, unatarajiwa kunufaisha wakazi 6,473 wa vijiji vya Fella, Geleka na Bujingwa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, mhandisi wa maji wa halmashauri hiyo, Ali Mruma alisema tayari maji yameanza kutoka na zinahitajika zaidi ya Sh3.8 milioni kununulia mashine ya kuyasukuma ili kuongeza usambazaji wa huduma kwa wananchi.

Diwani wa viti maalum, Christina Nyanda alisema maji hayo kata ya Mamaye yanatoka kwa kusuasua na kutaka wataalamu kutoa maelezo sahihi.

Mkandarasi wa kampuni la Cowi Tanzania Ltd inayotekeleza mradi huo, Ernest Tinka alikiri kuwapo upungufu na kuahidi kurekebishwa.