Kivuko MV Nyerere chalazwa ubavu

Muonekano wa awali baada ya kivuko cha Mv Nyerere kuanza kunyanyuliwa jana Septemba 24.

Muktasari:

Matumaini yameanza kuonekana katika kazi ya kukinyanyua na kukigeuza kivuko cha Mv Nyerere baada ya wataalam wa uokoaji kufanikiwa kukilaza ubavu huku wakiendelea na juhudi za kukinyanyua. Kivuko hicho kilizama Septemba 20, 2018


Ukara. Matumaini ya kazi ya kukinyanyua na kukigeuza kivuko cha Mv Nyerere yameanza kuonekana baada ya wataalam wa uokoaji kufanikiwa kukilaza ubavu.

Hadi jana jioni Septemba 24, 2018 kivuko hicho kilichozama mchana wa Septemba 20, 2018 kilianza kuonekana sehemu kubwa ambayo awali ilikuwa majini kutokana na vifaa mbalimbali kuingizwa majini na kutumika kukinyanyua.

Kazi ya kukinyanyua na kukigeuza kivuko hicho chenye tani 25 na uwezo wa kupakia abiria 101 na magari matatu ilianza juzi ikifanywa na wataalam kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na wenzao kutoka kampuni ya Songoro Marines ya jijini Mwanza.

Akizungumzia kazi hiyo mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo amesema kazi hiyo itafanyika kwa kasi na weledi kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kukinyanyua  mapema kabla ya wiki moja iliyotangazwa awali.

Wataalam kutoka vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Polisi,  Magereza na Uhamiaji pia wanashiriki kazi hiyo.

Akizungumza jana jioni, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mv Nyerere amesema kuna matumini makubwa ya kazi hiyo kukamilika mapema kabla ya makadirio ya siku saba iliyotolewa  na wataalam kutoka Songoro Marines.

Soma Zaidi: