Kivuko Mv Nyerere chahamishiwa Kigongo Feri

Muktasari:

Kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka Septemba 20, 2018 kisiwani Ukara, wilaya ya Ukerewe jijini Mwanza, kimehamishiwa Kigongo Feri


Misungwi.  Kivuko cha MV Nyerere kilichopinduka na kusababisha vifo vya watu 230 na manusura 41 eneo la kijiji cha Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, jijini Mwanza, kimehamishiwa eneo la Kigongo Feri, wilaya ya Misungwi jijini humo.

Kivuko hicho kimehamishiwa eneo hilo tangu usiku wa Oktoba 13, 2018 na kuegeshwa eneo hilo bila wengi kujua kutokana na maneno ya Mv Nyerere kufutwa kwa rangi ya kupulizia.

Ingawa hakuna kiongozi wa Serikali mkoani Mwanza aliyepatikana kuzungumzia kuhamishwa kwa kivuko hicho, waandishi wa Mwananchi waliofika eneo la Kigongo Ferry wamekishuhudia kikiwa kimeegeshwa hapo.

Akizungumza na Mwananchi juzi Jumatatu Oktoba 16, 2018, Mwenyekiti wa kijiji cha Bwisya, wilayani Ukerewe, Oru Mageru amesema hakuona wakati kivuko hicho kikiondolewa bali waliamka na hawakukikuta.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, Mkuu wa wilaya ya Misungwi kilipo kivuko hicho kwa sasa, Juma Sweda hawakupatikana kuzungumzia suala hilo baada ya simu zao za kiganjani kuita bila kupokelewa.

Hata waandishi wetu waliofika ofisini kwa Mongella hawakufanikiwa kuonana naye baada ya kuelezwa kuwa viongozi hao wanahudhuria kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa, RCC.

Kivuko cha Mv Nyerere kilipinduka Septemba 20, 2018 ambapo miili ya watu 230 iliopolewa huku wengine 41 wakiokolewa hai.