Kivuko kilibeba watu 265, waliofariki wafika 224

Zoezi la uopoaji wa Miili ya watu waliofariki katika ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere likiendelea.

Muktasari:

  • Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe ametoa taarifa za Kivuko cha MV Nyerere kwamba siku ya ajali kilibeba watu 265 wakati uwezo wake ni abiria 101

Dar es Salaa. Miili ya watu waliofariki katika ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere imeongezeka na kufikia 224 huku kivuko hicho kikiwa kimebeba watu 265 wakati kina uwezo wa kubeba watu 101.

Akitoa taarifa za ajali hiyo leo Septemba 23, 2018, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema licha ya kivuko hicho kuwa na uwezo wa kubeba abiria 101 siku ya ajali kilikuwa kimebeba abiria 265.

Waziri Kamwelwe amesema hayo mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika shughuli ya mazishi katika eneo la Shule ya Sekondari Bwisya.

Akitoa mchanganuo wa vifo, Waziri Kamwelwe amesema wanawake 126, wanaume 71, watoto wa kike 17, watoto wa kiume 10 na kufanya jumla ya maiti 224.

Amesema miili 219 iliyotambuliwa yote ilichukuliwa na kwenda kuzikwa na ndugu zao, wanne walikuwa hawajatambuliwa na wamechukuliwa vipimo vya DNA ili ndugu zao watakapofika waweze kutambua kuwa wamepoteza ndugu.

"Miili mingine mitano iliyotambuliwa ndugu zao waliamua kuungana nasi katika mazishi haya lakini kuna huyo mmoja tuliyempata sasa hivi taratibu zitaendelea baadaye," amesema Kamwelwe.

Amesema ajali ilitokea Septemba 20, 2018 saa 7.48 mchana na saa 8.10 mchana taarifa zilifika kwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliyekuwa katika kikao cha ulinzi na usalama na saa 10 jioni yeye na kamati hyo waliwasili eneo la tukio na kukuta wananchi tayari wameokoa watu 40.

Idadi ya 265 inatokana na waliofariki kuwa 224 na waliookolewa 41. Hata hivyo, shughuli za uokoaji zinaendelea.

Kuhusu michango inayotolewa, amesema, "Mpaka sasa pesa zilizochangwa na wananchi ni Sh190 milioni ili kusaidia katika shughuli hizi.”

“Mbali na hilo Serikali pia iko katika mpango wa kununua vivuko salama ili wananchi waweze kuendelea na shughuli za kiuchumi," ameongeza.

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira, Jenista Mhagama amesema baada ya mazishi Serikali itahakikisha inarejesha hali ya eneo hilo kwa kujihakikishia wamemaliza miili yote katika kivuko.

"Lazima tuhakikishe imetambulika, imezikwa lakini hata ile ambayo haijatambuliwa inahifadhiwa kwa upande wa Wizara ya Uchukuzi wahakikishe kivuko chetu kinarudishwa nchi kavu na kufanyiwa matengenezo,” amesema.