Kivuli cha Profesa Muhongo kutikisa Bunge

Muktasari:

Kuanzia wiki inayoanzia kesho, jina hilo linataraji kurudi tena bungeni, lakini safari hii ni kivuli chake tu ndicho kitatikisa Bunge, huku yeye mwenyewe akiwa anahudhuria vikao hivyo katika nafasi ya ubunge.

Dodoma. Jina la Profesa Sospeter Muhongo lilitawala wiki hii kutokana na sakata la mchanga wa dhahabu. Unaweza kuwa unakosea ukidhani mjadala huo umekwisha.

Kuanzia wiki inayoanzia kesho, jina hilo linataraji kurudi tena bungeni, lakini safari hii ni kivuli chake tu ndicho kitatikisa Bunge, huku yeye mwenyewe akiwa anahudhuria vikao hivyo katika nafasi ya ubunge.

Mtikisiko huo wa bungeni unaanza kwa wizara mbili kuwasilisha bajeti zao, lakini Wizara ya Nishati na Madini itakuwa moto zaidi kutokana na sakata la mchanga wa dhahabu kuwa ndiyo ‘habari ya mjini’ mpaka sasa.

Wizara ya Nishati na Madini inayosubiriwa kwa hamu na wabunge, itawasilisha bajeti yake kwa siku mbili- Alhamisi na Ijumaa- huku kukiwa na giza nene kuhusu waziri atakayewasilisha bungeni bajeti hiyo, iwapo Rais atakuwa bado hajateua mbadala.

Hatua hiyo inatokana na Rais John Magufuli kumng’oa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Profesa Muhongo kutokana na kutosimamia vizuri usafirishaji wa mchanga wa dhahabu.

Kanuni za Bunge zinataka waziri ndiye awasilishe bajeti na si naibu wake, na kumekuwa na hisia kuwa kama Rais Magufuli atakuwa hajateua waziri mwingine hadi kufikia siku hiyo, huenda Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene ataiwasilisha.

Simbachawene aliwahi kuhudumu wizara hiyo katika mabadiliko ya mwisho ya Baraza la Mawaziri Serikali ya Awamu ya Nne.

Wizara hiyo imekuwa na historia ya kukumbwa na kashfa zilizosababisha ama mawaziri wake kujiuzulu au kung’olewa na Rais na kwa sehemu fulani ikiwa ni kutokana na shinikizo la Bunge.

Lakini safari hii, Profesa Muhongo ameng’olewa si kwa shinikizo la Bunge, bali ripoti ya tume aliyoiunda Rais Magufuli iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma kuchunguza kiwango cha dhahabu kwenye makontena yaliyozuiwa bandarini.

Tume hiyo ilisema kampuni ya Acacia inayomiliki migodi mitatu nchini ilitangaza kiwango cha chini madini yote yaliyo katika makontena 277 ambayo yalizuiwa kusafirishwa nje kwa amri ya Rais.

Matokeo ya tume hiyo yanaonyesha thamani ya madini yote yaliyomo ni kati ya Sh829.4 bilioni na Sh1.439 trilioni, tofauti na thamani iliyotolewa na Acacia ya Sh97.5 bilioni.

Tangu kutolewa kwa taarifa hiyo na kung’olewa kwa Profesa Muhongo kumekuwa na mijadala mizito nchini hususan katika mitandao ya kijamii, na mijadala hiyo inatarajia kuhamia kwa wabunge wiki inayoanza kesho mjini Dodoma.

Tayari uongozi wa Acacia umepinga matokeo ya tume hiyo ikiwamo thamani ya madini, kauli inayoungwa mkono na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wa zamani (1993-2005), Andrew Chenge.

Chenge, ambaye ni pia ni mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM) na mwenyekiti wa Bunge, ndiye anayetajwa kushiriki katika uandaaji wa mikataba ya madini inayolalamikiwa kati ya Serikali na wawekezaji.

“Lakini pia wakizipiga hesabu ukiniambia mimi ni trilioni, mimi nakataa kwa sababu I know it (nafahamu). Mie nafikiri kuna mahesabu wameyakosea,” alisema Chenge nje ya Bunge juzi.

Chenge alifafanua kuwa usafirishaji huo wa mchanga wa dhahabu haufanyiki kila mwezi, bali ni lazima mwekezaji akusanye mzigo wa kutosha na si kuweka kontena moja kwenye meli ambayo ni gharama.

Hata hivyo, Chenge alisema hayo yanayotokea sasa katika sekta ya madini kwa mchanga kusafirishwa nje yasingetokea kama Serikali ingetekeleza mapendekezo ya Jopo la Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (Teiti) chini ya Jaji Mark Bomani.

Kauli hii ya Chenge na kauli za wabunge wengine zinaashiria kuwa kuna jambo halijakaa sawa katika sakata hilo la mchanga wa dhahabu uliokuwa usafirishwe nje na litatikiza bajeti ya wizara hiyo.

Akizungumza nje ya viwanja vya Bunge Jumatano wiki iliyopita, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema suala la kuibiwa katika sekta ya madini, alilipigia kelele kuanzia mwaka 1999.

“Tangu mwaka 1998 tulipotunga Sheria ya Madini na mwaka 1997 tulitunga sheria mbili za fedha, tatizo kubwa lipo kwenye kitu nilichokiita ‘utatu haramu’ wa sheria,” alisema Lissu.

Lissu, ambaye ni mwanasheria na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema mwaka 1998 ilitungwa Sheria ya Madini iliyorekebishwa mwaka 2010 baada ya maoni ya Teiti.

“Sheria inasema sehemu ya madini watakayoshindwa kuyasafishia hapa watayapeleka nje ya nchi. Kwenye huo mchanga kuna shaba, cobalt, fedha na dhahabu kidogo sana,” alisema Lissu.

Alisema mikataba ya madini inasema kuwa madini mengine shaba, cobalt na fedha hayatozwi kodi na kusisitiza kuwa vifungu hivyo vibaya viko kwenye mkataba.

“Rais wetu kama kawaida yake ameshauriwa? Amejiingiza kwenye mgogoro mkubwa, anafikiri anapata sifa ndogondogo hapa. Haya mambo tumeyapigia kelele kwa miaka mingi,” alisema.

“Rais aanzie huko akitoka aje kwenye mikataba ya nchi kwa nchi aondoe hiyo mikataba, akishaondoa anakuwa hashtakiki nje, akimaliza hiyo aje ndani.”

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba alisema amefurahi kwa sababu jambo hilo lilikuwa kero na sugu kwa muda mrefu.

“Hili jambo si la Tanzania tu, bali la Afrika kwa sababu mfumo wa uchumi wa dunia sasa umekuwa ni kuzidhulumu nchi zinazoendelea. Na nchi zetu zina rasilimali nyingi hazikujaliwa teknolojia,” alisema.

Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia alisema kuna tetesi za muda mrefu kuwa kwenye mchanga kuna madini, lakini Watanzania wamefumbuliwa macho na dunia nzima.

“Tulikuwa tunaibiwa sana. Ushauri wangu tuanze wenyewe ndani ya Serikali, lakini pia na wale ambao wametudhulumu kwa muda wote huo kwa kweli lazima watulipe fidia,” alisema.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Zubeda Sakuru alisema wapo viongozi wastaafu waliokuwapo madarakani wakati hayo yanatendeka ambao wanapaswa kuwajibika.

Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde aliunga mkono hatua ya Serikali, lakini akataka hatua inayofuata iwe ni kubadili sheria ya madini ili rasilimali hiyo ilinufaishe Taifa.

Katika mitandao ya kijamii, kumekuwapo na mijadala mizito, huku wengi wakihofia suala hilo kupelekwa mahakamani.

Wizara ya Fedha na Uchumi

Mjadala mwingine ambao unaweza kulitikisa Bunge wiki ijayo ni bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo itawasilisha Jumanne Dk Philip Mpango na mjadala kuhitimishwa Jumatano.

Katika mijadala iliyotangulia hasa ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wabunge wengi walipaza sauti zao wakitaka kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika huduma za utalii ifutwe.

Kodi hiyo ambayo ilipitishwa mwaka jana inalalamikiwa kuwa imesababisha watalii wengi kusitisha safari za kuja na Tanzania na kwenda Kenya ambayo haina kodi hiyo.

Pia suala la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kulalamikiwa kuwakomoa na kuwanyanyasa wafanyabiashara ikiwamo kwenda kudai kodi na mtutu wa bunduki nalo linaweza kuibua mjadala ndani ya Bunge.

Bajeti nyingine itakayowasilishwa wiki hiyo ni ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambayo nayo inaweza kuibua mijadala hasa ajira kwa wageni na soko la pamoja la nchi wanachama za Afrika Mashariki (EAC).