Kiwanda cha Dangote chatozwa faini Sh15 mil

Muktasari:

Hatua hiyo imekuja baada ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina kutembelea kiwanda hicho na kushuhudia shughuli zinazofanyika.

Mtwara. Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc),  limekitoza faini ya Sh15 milioni Kiwanda cha Saruji cha Dangote kwa kosa la kuwapo kwa taka ngumu na kukosekana kwa choo cha wateja wao na kulazimika kujisaidia  porini.

Hatua hiyo imekuja baada ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina kutembelea kiwanda hicho na kushuhudia shughuli zinazofanyika.

Mratibu wa Nemc Kanda ya Kusini, Lewis Nzila alisema kutokana na kiwanda hicho kukiuka sheria za mazingira wanalazimika kulipa faini hiyo ndani ya siku saba na kujenga choo cha muda ndani ya wiki mbili na kutengeneza maegesho ya magari ya mizigo ili kuepukana na vumbi.

 Awali, Mpina alitaka vyoo vya muda vijengwe ndani ya siku 14 na kulipa faini ndani ya siku saba.

Mkuu wa Idara ya rasilimali Watu kiwandani hapo, Kajele James alisema watatekeleza maagizo yote yaliyotolewa.