Kizaazaa saa nne za kukosekana kwa mwendokasi Dar

Muktasari:

Wananchi walalamikia ubovu wa miundombinu

Dar es Salaam. Saa nne za kukosekana kwa huduma ya mabasi yaendayo haraka maarufu ‘mwendokasi’ jana zilizua kizaazaa jijini Dar es Salaam baada ya wakazi wa viunga hivyo kulazimika kutembea umbali mrefu kwa miguu.

Kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa tatu asubuhi vituo vyote vya mwendokasi havikuwa na abiria, baada ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (UDart), kusitisha huduma za usafiri kutokana na kufungwa kwa Barabara ya Morogoro.

Baadhi ya wananchi mbalimbali waliozungumza na gazeti hili walilalamikia miundombinu korofi ya eneo hilo kuwa sababu ya kukosekana kwa usafiri pindi mvua kubwa zinaponyesha.

“Barabara zipitazo juu ndiyo suluhisho hapa jangwani, la sivyo kila mwaka hali itakuwa hivihivi. Leo hapa pikipiki zinaanguka, daladala hazipiti mpaka sasa hatujafika makazini, hii adha inajulikana na sidhani kama ni kitu kigeni, kimezoeleka Serikali ifanye jambo kunusuru hali hii,” alisema mkazi wa Magomeni Jamila Faiz.

Mkazi wa Mwembechai, Frank Ngatenga alisema: “Serikali haijagundua tatizo la hapa, inabidi wakae wajipange namna ya kutatua. Kujaa kwa maji mengi kumetokana na majengo yaliyojengwa hapa ya mwendokasi, maji yanashindwa kwa kupita.”

Barabara za Udart zilivyotumika

Baadhi ya magari madogo, daladala na bodaboda jana asubuhi zilitumia fursa hiyo kupitisha magari yao katika barabara zinazotumika na mabasi ya mwendokasi.

Mwananchi lilishuhudia daladala zikipita katika vituo hivyo kushusha na kupakia abiria huku trafiki wakielekeza baadhi ya magari kutoka kwenye barabara hizo.

Dereva wa daladala linalofanya safari zake Mbagala Rangitatu- Simu 2000 Jafari Himid alisema kutokana na foleni iliyopo, waliamua kutumia barabara za mwendokasi ili kuokoa muda.

Ofisi za Udart zahamishwa

Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Udart, Deus Bugaywa alisema: “Tumehamishia ofisi zetu Gerezani ili kuwezesha shughuli zingine za kiofisi kuendelea kwa sababu tangu saa nane usiku maji yameanza kujaa, tukaanza kutoa magari, saa 10 barabara ikawa imefungwa.”

Alisema jana saa tatu asubuhi ndipo huduma ya mwendokasi ilirejea.

Zimamoto wafanya uokoaji

Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambaye pia ni Kaimu Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mabusi Peter alisema usiku wa kuamkia jana walifanya uokoaji kwa familia ya watu zaidi ya watano eneo la Gongo la Mboto Ulongoni.

“Nyumba hiyo ambayo ipo eneo la mtoni ilizingirwa na maji na baadaye mwanaume mmoja na mtoto wa miezi sita waliokolewa baada ya kusombwa na maji,” alisema Kamanda Peter.